Kamati ya Utalii ya Jiji la
Mbeya iliyopo chini ya Halmashauri ya Jiji kupitia kwa Afisa Utalii Bi.Levina
Modest jana ilifanya ziara ya kitalii kuitembelea Shule ya Sekondari Iyunga
iliyopo Mkoani hapo kwa kushirikiana na wadau wakubwa wa masuala ya Utalii
Jijini Mbeya, Uyole Cultural Tourism Enterprises chini ya Mratibu wake Amos
Mwamugobole na Asasi nyingine isiyo ya kiserikali iitwayo ELIMISHA chini ya
Mkurugenzi wake Bw.Festo Sikagonamo.
Katika Ziara hiyo wajumbe wa
Kamati walionyeshwa Vitu mbalimbali vilivyotengenezwa toka enzi za Mkoloni
Mjerumani. Akiongea kwa bashasha kuu Mwalimu mwandamizi wa Michezo,Habari na
Utamaduni Sekondari ya Iyunga, Mwalimu Emmanuel Michael ameelezea kwa marefu
kuhusu kumbukumbu za kale zilizopo shuleni hapo ikiwemo kengere ya
kale,birika,bwawa la kuogelea,mahandaki kwa ajili ya ulinzi,kiti cha kukaa cha
kale,matanki ya maji pamoja na majengo vyote vikiwa vilitengenezwa mnamo mwaka
1925.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya
Utalii ,ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Sisimba Mhe.Geofrey Kajigili amemuomba
Mwalimu Michael kwa niaba ya Uongozi wa Shule hiyo kushirikiana na Kamati hiyo
ili kupata Wazee wa zamani waiishio maeneo hayo ili waweze kupata historia
nyingine nyingi kuhusu Utawala wa Kikoloni na taarifa zingine za kina.
Naye Afisa Utalii Bi.Levina
amesema kuna kila sababu ya kuboresha mazingira ya Shule hiyo ili yawe ya
Kitalii zaidi kwani yataisaidia Halmashauri kujitangaza na kujiingizia mapato
huku Shule na wanajamii wa Sekondari ya Iyunga watanufaika pia kwa kuwa na
Vivutio hivyo.
Mwishowe, Mwalimu Emmanuel
Michael aliushukuru Uongozi wa Halmashauri ,Kamati ya Utalii kwa kuliona suala
la Utalii kuwa ni jema na kuamua kulishupalia na kuiahidi Kamati hiyo
kushirikiana nayo bega kwa bega katika kufanikisha suala hilo zuri huku
akiiomba Kamati utekelezaji mwema wa majukumu yake.
Kiti hiki cha kukalia ni moja ya kivutio
shuleni hapo kilitengenezwa zaidi ya miaka 90 iliyopita enzi za Utawala wa
Kikoloni wa Kijerumani.
Ukuta huu ulijengwa na Wajerumani pembezoni
mwa Mto Nzovwe kwa ajili ya Ulinzi na Usalama kwani chini ya Ukuta huu kuna
Handaki kubwa linalounganisha maeneo ya ndani ya shule na nje ya eneo hilo.
Hili ni birika la kale lililokuwa likitumika
na Utawala wa Kijerumani kwa ajili ya kuhifadhia maji na vitu vingine
vinavyofanana na hivyo ambalo Uongozi wa Shule ya Sekondari Iyunga wamelitunza
vizuri hadi hivi sasa.
Hiki ni kifaa kitumikacho Kuratibu masuala
mbalimbali kuhusu Hali ya Hewa (Stevenson Screen) kilichojengwa na kutumika
tangu enzi za mkoloni Mjerumani.
Jengo hili ni Ukumbi uliojengwa na Mkoloni
ambao ndani yake kuna Handaki linalotoka mpaka nje ya maeneo ya Shule hiyo, Juu
kulia karibu na dirisha ni Kengere ya Mkoloni inayotumia umeme iliyokuwa
ikitumika kutoa taarifa mbalimbali kama kuna hatari au kuita watu mkutanoni kwa
ajili ya kujuzwa yanayojiri.
Kamati ya Utalii ya Jiji, Waandishi wa Habari
pamoja na Mwalimu mwenyeji Mwl Emmanuel Michael wakiwa eneo lilipo Bwawa la
Kuogelea lililojengwa na Enzi za Mkoloni.
Afisa Habari wa Halmshauri ya Jiji la Mbeya
Bi.Jacqueline Msuya akitoka ndani ya Handaki pamoja na wajumbe wengine
waliokuwa wakizungukia maeneo ya utalii ndani ya Shule ya Sekondari ya Iyunga, Jijini
Mbeya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii na Diwani wa
Kata ya Sisimba Mhe.Geofrey Kajigili (wa kwanza kushoto) akiwa na Afisa Utalii
wa Jiji Bi.Levina Modest wakisikiliza kwa makini maelekezo kutoka kwa mwenyeji
wao Mwalimu Emmanuel Michael wa Sekondari ya Iyunga.
Mwalimu Emmanuel Michael, Mwalimu mwandamizi
wa Michezo, Habari na Utamaduni akielekeza jambo kwa wajumbe wa Kamati ya
Utalii ndani ya Handaki lililopo shuleni hapo.
Wajumbe wa Kamati,
Waandishi wa Habari na Mwalimu mwenyeji kwenye viunga vya Shule ya Sekondari
Iyunga.
Wajumbe wa Kamati ya Utalii wakifurahia mara
baada ya Kuelezwa mambo mbalimbali na kuyatembelea, hapa wakiwa kwenye pozi la
kuruka juu ndani ya Bwawa la Kuogelea lillilojengwa tangu Enzi za Mkoloni miaka
90 iliyopita.
No comments:
Post a Comment