KAMPUNI Ya huduma za kifedha kwa njia ya mtandao Vodacom M- Pesa imetangaza ushirikiano mpya na mashirika makubwa kumi ya bima nchini kupitia mfumo wao wa VodaBima kwa lengo la kushirikiana na Serikali katika kufikia lengo la kukuza upatikanaji wa bima kutoka kiwango cha asilimia 0.6 ya pato la Taifa (GDP,) na kufikia walau asilimia 5 ifikapo 2030.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya ushirikiano iliyokwenda na kauli mbiu ya 'Linda Chombo, Linda Mazima na Voda Bima' Mkurugenzi wa Vodacom M-Pesa Epimack Mbeteni amesema tangu kuzinduliwa kwa huduma hiyo mwaka huu, VodaBima imekuwa chachu ya upokeaji wa huduma za bima nchini kwa kutoa huduma hiyo kidigitali kwa watumiaji zaidi ya 50,000.
Amesema, wana mategemeo makubwa ya kiuchumi kwa taifa na jamii kwa ujumla kupitia ushirikiano huo uliohusisha kampuni za bima za Britam Insurance, Alliance Insurance, Jubilee Insurance, Zanzibar Insurance Corporation (ZIC,) Bumaco Insurance, National Insurance Corporation (NIC,) UAP Insurance, Sanlam Insurance, Heritage Insurance na Mayfair Insurance.
"Lengo kuu la Vodacom ilikuwa ni kurahisha huduma za bima kwa watanzania kupitia simu za mkononi. Tumeweza kupunguza gharama za upatikanaji kwa bima na kurahisha mchakato mzima wa kuuweka kwenye mfumo wa M-Pesa na leo tunawapatia VodaBima iliyoboreshwa ambayo ni kubwa na yenye huduma nyingi....kwa kushirikiana na makampuni mengi zaidi ya bima kwenye mfumo wa VodaBima tutegemee mapinduzi makubwa ya teknolojia na Maendeleo ya kiuchumi." Amesema Mbeteni.
Aidha amesema, Serikali imeanzisha mfumo wa kutoa stika za kidigitali na kupitia VodaBima wateja watapata fursa ya kulipa kidogo kidogo kupitia akaunti zao za VodaBima mwaka mzima na kupatiwa ujumbe pale ambapo bima zao zinapokaribia kuisha muda wake.
"Tunawashukuru washirika wetu wapya na tunategemea kuwa huduma hii mpya itaongeza matumizi ya bima nchini.....na kwakuwa bima kubwa inapatikana kwenye VodaBima na tuna watoa huduma wengi zaidi sasa watumiaji wanaweza kununua bima zao na kufuatilia malipo kutoka popote nchini bila kufika katika ofisi za mawakala. Hii ni hatua moja zaidi katika safari yetu ya kuleta mabadiliko ya kidigitali nchini." Amesema.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni 10 za bima Mwenyekiti wa Chama cha Watoa huduma ya Bima Tanzania Hamis Suleiman amesema Vodacom Tanzania wamekuwa wabunifu katika kukuza teknolojia ya mawasiliano nchini.
"Tunachokiona leo ni matokeo ya ushirikiano unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za bima kwa watanzania, tunatumia mtandao mpana wa Vodacom kutimiza mahitaji ya soko na ninaamini kuwa ushirikiano huu utatuleta karibu zaidi na malengo yetu ya bima nchini." Ameeleza Suleiman.
Kwa upande wake kamishina wa Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania Dkt. Mussa Juma amesema dhamira yao ni kujenga, kutetea na kuendeleza soko jumuishi lenye tija na salama kwa watumiaji wa bima.
"Tunafurahi kuona wadau wa mashirika binafsi wakileta ubunifu kwa utoaji wa huduma za bima kwa Taifa, Vodacom ni mfano wa kuigwa na litaongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa matumizi ya huduma za bima nchini." Amesema.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Meneja masoko na huduma za kifedha kutoka Vodacom Noel Mazoya amesema kampuni hiyo imejizatiti kupeleka taifa katika matumizi ya fedha kidigitali.
Amesema walianza na shirika la Bima la Britam na sasa wana washirika 10 watakaojenga ushirikiano mkubwa utakaoioeleka Tanzania mbele katika kukuza uchumi na sekta ya bima kwa ujumla.
Matukio mbalimbali ya uzinduzi rasmi wa ushirikiano baina ya Vodacom M-Pesa na kampuni 10 za bima.
Mkurugenzi wa huduma za M-Pesa Epimack Mbeteni akifuatili mawasilisho ya wadau mbalimbali wa bima kupitia mtandao huo.
Mwenyekiti wa Chama cha wamiliki wa Bima Khamis Suleimani akizungumza katika hafla hiyo na kueleza kuwa wataendelea kutumia mtandao mkubwa wa Vodacom katika kutimiza mahitaji ya soko, leo jijini Dae es Salaam.
Kamishina wa Bima Tanzania Dkt. Mussa Juma akizungumza wakati wa hafla hiyo na kuipongeza kampuni ya teknolojia na mawasiliano Vodacom kwa kuendelea kuwa kinara wa matumizi ya kidijitali nchini, leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Bima Tanzania Khadija Said akifuatilia mjadala wakati wa uzinduzi rasmi wa ushirikiano baina ya Vodacom M-Pesa na kampuni kumi za bima leo jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment