Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji akipewa maelezo na
Meneja Msaidizi upande wa Ukaguzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Bw. Mustapha Mkiramweri alipofanya ziara ya kushitukiza katika mmoja wa
mitaa Jijini Dodoma, kusikiliza kero za wafanyabiashara zinazoelekezwa
kwenye Mamlaka ya Mapato TRA mkoa wa Dodoma.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji akipewa maelezo na Meneja
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Thomas Masese (kulia)
alipokuwa akifanya ziara ya kuwatembelea wafanyabiashara na kujua
changamoto wanazokumbana nazo kutoka kwa TRA mkoani Dodoma.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji akiwa na Watumishi wa
Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA), wakisikiliza malalamiko ya mteja
kwa njia ya simu walipomtembelea ofisini kwake kujua changamoto
wanazokumbana nazo kutoka kwa TRA mkoani Dodoma, baada ya mfanyabiashara
huyo kuilalamikia TRA kumlazimisha kununua mashine za kutolea
stakabadhi ya kielektroniki (EFD Machine)
Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kumsimamisha kazi maramoja mfanyakazi wake mmoja katika Ofisi ya TRA mkoa wa Dodoma, DANIEL KINGU, kupisha uchunguzi wa kuhusika kwake na tuhuma zinazomkabili za kumbughudhi mfanyabiashara mmoja Jijini humo.
Dkt. Kijaji, ametoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya kushitukiza kwenye mitaa ya Jiji la Dodoma baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara mmoja kwamba amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa mfanyakazi huyo akishirikiana na watu wengine na kumtaka ampelekee shilingi laki 7 za kulipia mashine ya kutolea stakabadhi za kielektroniki (EFD Machine) la sivyo angefungiwa biashara yake.
“Mteja wetu awe salama!! na nitaendelea kufuatilia, lakini kuanzia muda huu Kingu aondoke ofisini, hatuwezi kuwavumilia watu wa jinsi hii hata kidogo kwa sababu kazi ya kuuza EFD machine si yake na anamwambia mteja aende ofisini kwake chumba namba fulani, anafanya haya mambo ndani ya ofisi ya Serikali, akitoka nje inakuwaje?” alihoji Dkt. Kijaji
Alisema hatasita kuchukua hatua hizo kwa wafanyakazi wengine wa Mamlaka ya Mapato popote walipo nchini wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili.
Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango, amewataka watendaji wa TRA nchini kote kufanyakazi zao kwa kuzingatia maadili yao ya kazi, kukadiria kodi kwa haki, watumie lugha nzuri kwa wateja wao na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa wafanyabiashara katika masuala ya kodi badala ya kuwakadiria kodi kubwa isiyolipika.
“Ni lazima tuwalee wafanyabiashara hawa wadogo na ndio watakaotulipa kodi kubwa huko mbeleni badala ya kuwaumiza tangu wanapoanza biashara zao na ni lazima tuangalie viwango vyetu vya kodi tunavyotoza” Alisisitiza Dkt. Kijaji
Meneja wa TRA mkoa wa Dodoma, Bw. Thomas Masese, ameahidi kutekeleza maagizo hayo na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo huku naye akirejea wito kwa watumishi wa Mamlaka hiyo mkoani humo, kufanyakazi zao bila kuwanyanyasa wafanyabiashara pamoja na kutohusisha na vitendo visivyofaa ikiwemo kuomba rushwa
No comments:
Post a Comment