MAKAMU WA RAIS AKOSHWA NA UTENDAJI WA DAWASA, AHAIDI KUWAPA MIRADI MINGI ZAIDI NCHINI - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Sunday, February 14, 2021

MAKAMU WA RAIS AKOSHWA NA UTENDAJI WA DAWASA, AHAIDI KUWAPA MIRADI MINGI ZAIDI NCHINI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameonyesha kufurahishwa na kazi kubwa na nzuri wanayoifanya na DAWASA ya usimamizi wa miradi na kusogeza huduma ya Maji kwa wananchi wengi ambapo ameahidi kufikiria kuwapa miradi iliyo nje ya Jiji la Dar es salaam.

Mhe. Samia ametoa kauli hiyo wakati wa ukaguzi wa Mradi wa Usambazaji wa Maji Kisarawe II, Wilaya ya Kigamboni ambao amesema kwa uwezo walioonyesha DAWASA anaamini ifikapo 2025 upatikanaji wa maji Jiji la Dar es salaam utakuwa ni 100%.


Aidha Mama Samia amewataka wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya Maji Jijini humo kuzingatia mikataba kwa kuhakikisha Miradi inakamilika ndani ya muda uliopangwa ili iweze kutatua kero za wananchi.

Pamoja na hayo amewaelekeza Viongozi wa Mitaa kuhakikisha wanaunda Kamati za Maji kwaajili ya kulinda miundombinu ya Maji, kuwaripoti wale wanaobainika kuiba au kuharibu miundombinu ya Maji na kuwahamasisha wananchi kulipia bili zao kwa wakati.

Nae Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso amesema utendaji kazi mzuri wa DAWASA ndio umepelekea Mamlaka hiyo Sasa kuanza kupewa Miradi mikubwa Mikoani kama vile mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe sababu wameonyesha uwezo mkubwa hivyo amemtaka Mtendaji Mkuu wa DAWASA kuhakikisha anaendelea kufanya kazi kwa bidii.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema hadi kufikia Sasa Visima 7 Kati ya 12 vinavyojengwa eneo la Kimbiji vimekamilika na vitakuwa na uwezo wa kuzalisha Lita milioni 57.9 kwa hivyo vitaweza kuhudumia Wilaya yote ya Kigamboni na maeneo ya Kongowe na Mbagala hivyo kufanya tatizo la uhaba wa Maji Kigamboni kubaki historia.

Ukaguzi wa utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji wa Maji Kigamboni umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Watendaji wa Wizara ya Maji, Wastahiki Meya,Vyombo vya ulinzi na usalama, Viongozi wa Wilaya, Chama Cha Mapinduzi, Madiwani na Wananchi.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages