
- Asema zoezi la kuhama linakwenda vizuri DSM.
- Awapongeza Machinga walioanza kuhamia kwenye maeneo rasmi.
- Ataka Barabara za mitaa Kariakoo zibaki wazi.
Zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kumalizika kwa muda wa mwezi mmoja uliotolewa kwa Wafanyabiashara wanaoendesha Biashara kwenye maeneo yasiyo rasmi kupangwa vizuri,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amewataka wote wanaofanya biashara Kwenye maeneo yaliyokatazwa kutumia Siku tatu zilizosalia kuhama ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
RC Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa Kikao kazi Cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Kuwapanga Machinga kwa kila Wilaya ambapo amesema kwa hizi siku tatu Serikali itaongeza Nguvu kwenye kutoa matangazo na elimu ili kuhakikisha ifikapo October 18 kila Mfanyabiashara awe kwenye eneo alilopangiwa.

Aidha RC Makalla amesema zoezi la kuwapanga linakwenda vizuri Kufuatia Wafanyabiashara kupata elimu ambapo amewapongeza Viongozi wa Machinga na Machinga kwa kuchukuwa hatua mapema.
Hata hivyo RC Makalla amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala kuhakikisha Wafanyabiashara wote waliopanga meza Katikati ya Barabara za mitaa Kariakoo ikiwemo Msimbazi kuondolewa ili Barabara zibaki wazi magari yashushe Mizigo.
Pamoja na hayo RC Makalla amewapongeza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kwa kusimamia vizuri zoezi hilo.
RC Makalla pia ameelekeza maeneo yote watakayopelekwa Wafanyabiashara ikiwemo Masoko Daladala zishushe abiria kwenye maeneo hayo ili kuchochea Biashara.

Miongoni mwa Wafanyabiashara wanaotakiwa kupangwa ni Wale Waliojenga Vibanda juu ya Mitaro na mifereji, Wanaofanya biashara Kwenye maeneo ya watembea kwa miguu, wanaofanya biashara Kwenye hifadhi ya Barabara, Wanaofanya biashara mbele ya Maduka, na wanaofanya biashara Kwenye Taasisi za Umma zikiwemo shule.
No comments:
Post a Comment