
Na Mashaka Mhando, Muheza
HEKTA 8,000 za mazao mbalimbali wilayani Muheza, zimeshambuliwa na wadudu waharibifu wajulikanao kwa jina la Viwavijeshi.
Kufuatia hali hiyo, Mbunge wa Muheza Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA, ameishukuru serikali baada ya kumpa lita 86,000 za sumu aina ya Power-Cron itakayokabiliana na uharibifu huo.
Akizungumza wakati akizindua zoezi la usambazaji wa dawa hizo, alisema mara baada ya kutokea wadudu hao na wakulima kulalamika, alifikisha kilio chao kwa kuomba dawa yenye viuwatilifu vya kukabiliana na wadudu hao kwa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.
"Namshukuru Waziri Rais wetu Samia Suluhu Hassan, kiukweli dawa hii itatusaidia kupambana na wadudu hawa mashambani," alisema mbunge.

Hata hivyo, mbunge alisema anapanga kukutana na makundi ya wakulima ili aweze kuzungumza nao kutazama namna ya kutatua changamoto zao.
"Nataka kukutana na wakulima lengo ni kuwabadilishia maisha yawe bora zaidi kuliko jana na leo, kwa kuzalisha mazao bora na masoko ya uhakika," alisema MwanaFA.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Muheza, Erasto Mhina amemshukuru mbunge kwa jitihada za kupata dawa hiyo ambayo itaokoa mazao yalikuwa yameshambuliwa na wadudu hao.
Ofisa Kilimo wilayani Muheza, Hoyange Mbwambo, alisema kuwa sumu hiyo aina ya Power-Cron imeanza kusambazwa kwa wakulima ili kukabiliana na wadudu hao waharibifu.
Hata hivyo, ofisa huyo alisema pamoja na wadudu kushambulia mazao ya wakulima lipo tatizo la ukosefu wa mvua mwaka huu linalotishia upungufu wa chakula.

No comments:
Post a Comment