
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa muda Maalum kuanza kwa ujenzi wa Masoko ya Chuini pamoja na Jumbi yaliyokaa kwa muda mrefu bila ya kuanza kwa ujenzi.
Mhe. Hemed ametoa agizo hilo katika ziara ya kukagua ujenzi wa Miradi ya Masoko ndani ya Mkoa wa Mjini Magharib.
Amesema hajafurahishwa na hatua iliyofikia katika Soko la Chuini na kueleza kuwa Taarifa za Ujenzi huo zilizotolewa na Muwekezaji na Mkandarasi sio za kuridhisha ambapo ameuagiza Uongozi wa Afisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kuhakikisha wanakaa na Muwekezaji ndani ya wiki mbili ujenzi huo uanze.

Katika ujenzi wa Soko la Jumbi Mhe. Hemed ametoa Mwezi Mmoja kwa Mkandarasi kuanza ujenzi katika soko hilo na kumtaka mara moja kuanza kusafisha eneo hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema uwepo wa Masoko hayo itasaidia kustawisha hali za Wananchi na Wafanyabiashara kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi ambapo wataweza kukuza kipato Chao na Serikali kuweza kukusanya mapato kwa kukuza Uchumi wa Nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Nchini Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Muhamed ameeleza kuwa Wizara kupitia Serikali ya Wilaya na Serikali ya Mkoa wamekuwa mstari wa mbele kusimamia na kufuatilia ujenzi huo na kueleza kuwa jitihada za Wizara ni kutaka kukamilika Masoko hayo kwa maslahi ya Wananchi.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Serikali ya Mkoa imekuwa ikifanya ukaguzi wa maeneo hayo mara kwa mara ambapo ilifanya jitihada ya kuwaita wawekezaji wa Soko la Chuini ambapo Wawekezaji hao wameonesha kudharau wito huo jambo ambalo serikali ya Mkoa haitoweza kulivumilia.
Awali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametembelea ujenzi wa Darajani Bazar na kueleza kuridhishwa kwake kwa hatua iliyofikia ambapo ameeleza kuwa eneo hiloi ni kitovu cha biashara Nchini na amewahikishia Wananchi kukamilika kwa ujenzi huo Serikali itasimamia utoaji wa maduka hayo kwa kufuata utaratibu utakaopangwa bila ya upendeleo.

No comments:
Post a Comment