Mhe Hemed akiahirisha Mkutano wa 8 wa Baraza la 10 la Wawakilishi Chukwani - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Friday, September 30, 2022

Mhe Hemed akiahirisha Mkutano wa 8 wa Baraza la 10 la Wawakilishi Chukwani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akikihairisha Mkutano wa 8 wa Baraza la 10 la Wawakilishi Chukwani jijini Zanzibar Leo tarehe 30.09.2022

Serikali imeamua kuyajenga Masoko ya Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini kwa kupitia vikosi vya Idara Maalum za SMZ ili kuwaondoshea usumbufu uliodumu kwa muda mrefu wananchi wake.

Makamu wa pili wa Rasi wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abulla ameyasema hayo wakati akiakhirisha mkutano wa Nane (8) wa baraza la Kumi (10) la Wawakilishi Chukwani nje kidogo wa mji wa Zanzibar.

Amesema kuwa Serikali imeamua kukabidhi Miradi ya ujenzi wa Masoko hayo kwa Vikosi vya Idara Maalum za SMZ ambapo hapo awali walikabidhiwa wakandarasi wazawa na kuonesha kusuasua kwa ujenzi huo kwa muda mrefu jambo ambalo linawaletea usumbufu wananchi wake.

Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali imeamua kufanya hivyo ili kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi wake ambapo Soko la Mwanakwerekwe litajengwa na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Soko la Jumbi litajengwa na Chuo cha Mafunzo na Soko la Chuini litajengwa na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi (KZU).

Aidha, Mhe.Hemed amesema kuwa katika kuboresha sekta ya miundombinu Serikali imeingia mkataba wa ujenzi wa barabara wa kilomita Mia Moja nukta tisa (100.9) na kampuni ya China Civil Engineering Corporation (CCECC) ujenzi huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni utachukua kipindi cha miezi Thelathini na sita (36) hadi kukamilika kwake na utagharimu kiasi cha Dola za kimarekani Milioni Mia Moja na kumi na sita (116).

Amesema, Ujenzi huo unahusisha Ujenzi wa Barabara za Mjini kwa kiwango cha lami, zitakazokuwa na njia za waendao kwa miguu, kuekwa taa za barabarani, misingi ya maji ya mvua pamoja na bustani. Aidha, ujenzi huo utajumuisha na ujenzi wa barabara za juu (fly over) katika eneo la makutano ya barabara za Amani na Mwanakwerekwe kwa lengo la kuzifanya barabara hizo kuwa za kisasa na kuimarisha haiba ya Mji wa Zanzibar, ili uendane na hadhi ya Miji ya Kitalii.

Mhe. Hemed amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nane (8) inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 ibara ya 165, MKUZA III, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar (Vision 2050) pamoja na Mpango Kabambe wa Usafirishaji wa Zanzibar (Zanzibar Transport Masterplan).

Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa kupitia ripoti iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonesha kuwepo wa matumizi mabaya ya fedha za umma,Ufisadi, Rushwa, na Wizi kwa baadhi ya watendaji hivyo, amewataka Viongozi wenye dhamana kuwasimamia watendaji walio chini ya dhamana zao ili kuvidhibiti vitendo hivyo.

Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali haitakua na muhali wa aina yoyote kwa mtendaji atakaebainika anafanya mambo kinyume na taratibu za nchi yetu, hii itaambatana na hatua kali zitakazochukuliwa dhidi ya wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivi na Serikali haitamuonea mtu yeyote katika hili kwani uchunguzi wa kina utafanywa kuhakikisha haki inatendeka.

Makamu wa Pili wa Rais amewataka watendaji wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kuendelea kufanya kazi zao kwa weledi ikiwemo kuipitia Ripoti ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuangalia wale wote waliohusika na makosa mbali mbali ya Rushwa na Uhujumu wa Uchumi ili kuweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria No. 1/2012 ya makosa ya uhujumu Uchumi Nchini kwani makosa mengi ambayo yameripotiwa ni pamoja na kuomba na kupokea Rushwa kinyume na Kifungu cha Thelathini na Sita (36), ubadhirifu wa mali na mapato kinyume na Kifungu cha 42(1)(a), kutumia vibaya mali kinyume na Kifungu cha 43, matumizi mabaya ya Ofisi kinyume na Kifungu cha 53, kukwepa kulipa kodi kinyume na kifungu cha 44 na magendo kinyume na Kifungu cha 45.

Pia Mhe. Hemed amewatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa ZAECA inafanyakazi zake kwa misingi ya Sheria, haki na uadilifu na hakuna mtu yeyote atakaeonewa. “natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha ZAECA inatimiza majukumu yake ipasavyo ili nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali iweze kurudi” amesema

Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa pato la nchi kwa kwa mwaka 2022 limeongezeka kwa asilimia (20.8%) ukilinganisha 2020- 2021 ambapo nchi ilikubwa na janga la Uviko 19 hali iliyosababisha uchumi wa dunia nzima kushuka, amesema kwa sasa Serikali imeelekeza nguvu zake katika kuongeza makusanyo hususan kupitia vyanzo vya mapato yasiyokua ya kodi sehemu ambayo Serikali ilikuwa haifanyi vizuri kutokana na uvujaji mkubwa uliokuwa ukijitokeza kupitia wafanyakazi wetu wasio waaminifu.

Amesema kuwa Serikali imeamua kutumia mfumo wa makusanyo wa kielektroniki wa ZANMALIPO ili kupunguza mianya ya uvujaji na kuongeza mapato ya nchi. Hivyo, Mhe. Hemed amewaagiza watendaji wote wanaohusika na ukusanyaji wa mapato kutumia mfumo huo na kuhakikisha unalindwa ipasavyo ili usiweze kuchezewa.

Juhudi maalum zitaelekezwa katika kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kufanya vitendo vya wizi na ubadhirifu wa mali za umma ikiwemo wataalamu wanaoichezea mifumo yetu, aidha, ni jukumu letu sote kuhakikisha mapato yote yanakusanywa vizuri kwa kushirikiana na mamlaka husika” amesema.

Akizungumzia kuongezeka kwa watalii nchini Mhe. Hemed amesema kuwa kuna ongezeko la watalii Laki Moja na Thelathini na Tatu, Mia Tano na Arobaini na Moja (133,541) na kufikia watalii Laki Tatu Tisini na Nne, Mia Moja na Thamanini na Tano (394,185) kwa mwaka 2021 kutoka watalii Laki Mbili na Sitini, Mia Sita na Arobaini na Nne (260,644) kwa mwaka 2020. Amesema hii inatokana na amani na utulivu iliopo nchini pamoja na utoaji wa huduma zilizo bora na za haraka katika Viwanja vya Ndege, Bandari na Mahotelini.

Aidha, ametoa wito kwa Uongozi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kusimamia nidhamu, mila, silka, tamaduni na maadili ya nchi yetu kwa watalii wote wanaoingia nchini. Sambamba na hilo, amewataka kuchukua hatua kali kwa mtalii yeyote atakaekwenda kinyume na sheria na miongozo tuliyojiwekea kwa maslahi mapana ya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa serikali imeamua kuwaongezea mishahara wafanyakazi wake ili kuimarisha utawala bora na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zilizojitokeza katika zoezi hilo na kusema kuwa kila mafanyakazi atalipwa haki yake kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Mhe.Hemed amesema kuwa baada ya Serikali kuongeza mishahara kumezuka wafanyabiashara ambao si waaminifu na kuamua kuongeza bei za bidhaa kama vile Mchele, Sukari na Unga wa ngano kinyume na sheria jambo ambalo linaleta manung’uniko makubwa kwa wananchi hivyo ameiagiza Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kuwachukulia hatua kali wafanyabiashara hao kwa mujibu wa sheria.

Katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya Maji Safi na Salama Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali inatekeleza miradi mikubwa miwili ukiwemo mradi wa mkopo wa EXIM Bank wa Milioni Tisiini na Mbili nukta Moja Nane (92.18) ambazo zimepangwa kutumika kwa kumalizia uchimbaji wa Visima 64 matangi 15 na uungwaji wa mabomba katika Shehia 36 kwa Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini Unguja na hadi sasa ujenzi huo umeshafikia asilimia 62%.

Na mradi mwengine ni ule wa ahuweni ya Uviko 19 ambapo ZAWA imetengewa jumla ya shilingi Bilioni thelethini na Mbili nukta Mbili (32.2) ambazo zinatumia kwa uchimbaji wa visima thelathini na Nane (38) kwa Unguja na Pemba na kujumisha matengenezo ya visima 36 vya Ras el Khema na ujenzi matangi 10 kwa Unguja na Pemba pamoja na matengenezo ya Mtangi matatu (3) ya zamani.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa miradi yote inayojengwa kwa kutumia fedha za Ahueni ya UVIKO 19 iko katika katua za mwisho kukamilika kwake pamoja na vifaa ambavyo zinastahiki kuwemo kwenye miradi hio.

Akizungumzia huduma za Afya Mhe. Hemed amesema Serikali imejipanga kuleta madaktari bingwa kutoka pande mbali mbali za dunia kwa lengo la kuja kubadilishana uzoefu na madaktari wetu ili wananchi wapate huduma bora na zinazokwenda na wakati.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa huduma za afya zilizo bora kwa wananchi wake na kukabiliana na maradhi mbali mbali ya mripuko yanayojitokeza. “Nachukua fursa hii kuwaomba sana wananchi wenzangu ambao bado hawajawapeleka watoto wao kupata chanjo kuhakikisha wanawapeleka kupata huduma hiyo kwa kulinda Afya za watoto wao ambao ndio taifa la kesho”.

Katika kuakhirisha kikao hicho jumla ya Maswali ya Msingi Mia moja na Hamsini na Saba (157) na maswali ya nyongeza Mia Tatu na Sitini (360) yaliulizwa na yalijibiwa na Waheshimiwa Mawaziri. Pia katika mkutano huo jumla ya Miswada Miwili (2) imejadiliwa na kupitishwa. Miswada yenyewe ni:-

I. Mswada wa Kufuta Sheria ya Baraza la Wawakilishi (kinga, uwezo na fursa), Namba 4 ya mwaka 2007 na kutungwa Sheria mpya ya Baraza la Wawakilishi (kinga, uwezo na fursa) katika kutekeleza kazi na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

II. Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar na mambo yanayohusiana na hayo.

Kikao hicho cha Baraza la wawakilishi kimehairishwa hadi Siku ya Jumatano tarehe 23 Novemba, 2022 saa 3.00 kamili asubuhi.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages