DIRA MOJA, TAIFA MOJA: SMT NA SMZ ZAUNGANISHA NGUVU MILANGO YA AJIRA NA MAHUSIANO YA KAZI - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Tuesday, March 17, 2026

DIRA MOJA, TAIFA MOJA: SMT NA SMZ ZAUNGANISHA NGUVU MILANGO YA AJIRA NA MAHUSIANO YA KAZI

Na. OWM- KAM, Zanzibar

Katika kuonesha kielelezo cha juu cha mshikamano wa kidiplomasia na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimeingia katika ukurasa mpya wa mashirikiano yenye lengo la kupaisha sekta ya kazi, ajira, na mahusiano nchini.

Katika mazungumzo ya kiitifaki yaliyofanyika mjini Zanzibar, Machi 17, 2026,kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ), Mhe. Deus Sangu, na mwenyeji wake, Waziri wa Kazi na Uwekezaji wa SMZ, Mhe. Shariff Ali Shariff walikubalina kuimarisha urithi wa Muungano na kutafsiri maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Waziri Sangu alibainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imejipanga kuhakikisha fursa za ajira nje ya nchi zinawanufaisha vijana kote Bara na Visiwani bila ubaguzi.

Amesema tayari fursa za ajira nchini Qatar zimepatikana, na utaratibu wa kuwafikia vijana wa Zanzibar utajumuishwa kikamilifu. Hatua hii inalenga si tu kutoa ajira, bali kukuza hadhi na staha kwa wafanyakazi wa Kitanzania wanapokuwa nje ya mipaka, huku kipaumbele kikielekezwa katika kumuondolea mwanamke na kijana umaskini.

Eneo jingine la kimkakati lililoafikiwa ni ushirikiano katika utatuzi wa migogoro ya kazi kupitia Tume ya Usuluhishi na Utatuzi (CMA), pamoja na usimamiaji wa mkataba wa kazi za staha.

Waziri Sangu amesisitiza katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba ujenzi wa mahusiano hayo ni mwanzo wa safari ndefu ya kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa rafiki na yenye kulinda utu wa mfanyakazi kwa Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake, Waziri Shariff Ali Shariff amepongeza hatua hiyo ya kiungwana, akibainisha kuwa kuimarika kwa mashirikiano hayo ni tiba tosha ya kupunguza kero za Muungano na kuchochea ustawi wa kijamii.

Amesisitiza kuwa udugu wa kihistoria uliopo unapaswa kuonekana kwenye vitendo vya kiserikali na kuiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kuijumuisha Zanzibar katika majukwaa ya kimataifa kama SADC na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ili vyama vya wafanyakazi na waajiri Visiwani viweze kunufaika na fursa za kikanda.

Kufuatia mazungumzo hayo yenye tija, Mawaziri hao wawili wameafikiana haja ya kuwa vikao vya kitaalamu vya Makatibu Wakuu ambapo wameagiza vianze mapema mwezi Aprili, vifuatiwe na vikao vya ngazi ya Mawaziri ili kuanza utekelezaji wa haraka wa makubaliano ya ushirikiano.

Kikao hicho cha kihistoria kimehudhuriwa pia na viongozi waandamizi wakiwemo Katibu Mkuu SMZ, Khamis Suleiman Mwalim, na Naibu Katibu Mkuu OWM, Zuhura Yunus.

Waziri Sangu anahitimisha ziara yake ya siku moja Zanzibar kwa kushiriki hafla ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais waj Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi—tukio linaloashiria upendo na umoja wa kitaifa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages