
Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) Mkoa wa Dodoma, Jesca Nsamba, amesema wanawake wanaendelea kunufaika na mageuzi yanayofanyika katika sekta ya madini, huku akitoa pongezi kwa serikali kwa mchango wake mkubwa katika kukuza sekta hiyo.
Ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati wa kongamano la fursa na mageuzi kwa wanawake katika sekta ya madini, ambapo amebainisha kuwa wanawake wamekuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa juhudi hizo.
Ameeleza kuwa licha ya msaada unaotolewa na serikali, wanawake wamekuwa wakionyesha juhudi binafsi kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa bidii bila kusubiri kufanyiwa kila kitu na kupitia TAWOMA, wameendelea kuweka mikakati ya kuwainua wanawake ili waweze kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo katika sekta ya madini nchini.
Nsamba amesisitiza kuwa si muda mrefu tangu wanawake waanze kushiriki katika shughuli za madini, ambazo hapo awali zilionekana kuwa ni kazi za wanaume pekee, hata hivyo kwa sasa mafanikio yao yanaonekana wazi, huku wanawake wengi wakijitokeza na kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Amezitaja changamoto zinazowakabili wanawake katika sekta hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji na vifaa, akitoa wito kwa wadau na wafadhili kuongeza msaada zaidi ili kuwawezesha kufikia malengo yao, pia amewahimiza wanawake kuwa na ujasiri na kujiamini, akieleza kuwa wana uwezo mkubwa wa kufanikiwa katika sekta ya madini.

No comments:
Post a Comment