BENKI YA ABSA TANZANIA YATHIBITISHA KUJITOLEA KUWEZESHA WANAWAKE KATIKA TEKNOLOJIA KUPITIA GIRLCODE HACKATHON 2026 - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Monday, September 28, 2026

BENKI YA ABSA TANZANIA YATHIBITISHA KUJITOLEA KUWEZESHA WANAWAKE KATIKA TEKNOLOJIA KUPITIA GIRLCODE HACKATHON 2026

Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Oscar Mwamfwagasi, akizungumza na washiriki wakati wa hafla ya kufunga programu ya mwaka 2026 ya GirlCode Hackathon, jijini Dar es Salaam jana. GirlCode Hackathon ni sehemu ya mpango mpana wa GirlCode unaotekelezwa barani Afrika kwa lengo la kuwawezesha wanawake vijana kupata ujuzi wa vitendo katika teknolojia, ushauri elekezi pamoja na fursa za kuunda suluhisho zinazolenga kukabiliana na changamoto halisi katika jamii zao.

Benki ya Absa Tanzania imethibitisha tena dhamira yake ya kuwawezesha wanawake katika sekta ya teknolojia kufuatia kukamilika kwa mafanikio kwa GirlCode Hackathon 2026, shindano la siku mbili la ubunifu lililowakutanisha wasichana na wanawake vijana wenye ujuzi wa uandishi wa programu (coding), uendelezaji wa mifumo na ujasiriamali kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Katika program hiyo, iliyofanyika kwa ushirikiano na Neurotech, Sahara Ventures, Snippe, Sndbx Spaces na GirlCode Africa, iliwapa washiriki jukwaa la kubuni na kuendeleza suluhisho za kidijitali zinazolenga kutatua changamoto halisi katika maeneo ya teknolojia ya fedha (Fintech), Akili Bandia (AI) na usalama wa mtandao (cybersecurity).

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga shindano hilo iliyofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Oscar Mwamfwagasi, aliwapongeza washiriki kwa ubunifu wao, azma na uwezo wa kutatua changamoto.

“Suluhisho zenu ziliibuka si kwa sababu ya ubora wake wa kiteknolojia pekee, bali pia kutokana na uwezo wake wa kuleta mabadiliko halisi. Mmeweza kukabiliana na changamoto tata kwa ujasiri na ubunifu mkubwa, mkithibitisha kuwa ubunifu hauna mipaka ya kijinsia na kwamba mustakabali wa teknolojia ni angavu zaidi kwa sababu yenu,” alisema.

Bw. Mwamfwagasi alisema GirlCode Hackathon hiyo ilikuwa zaidi ya shindano, kwani ilikuwa jukwaa la kujifunza, kushirikiana, kukua na kuleta mabadiliko. Alibainisha kuwa washiriki waliweza kuandaa suluhisho mbalimbali, kuanzia majukwaa ya huduma za kibenki yanayounganisha mifumo mbalimbali hadi injini za uboreshaji zinazoendeshwa na Akili Bandia, jambo linaloonyesha uwezo wa wanawake vijana wa Kitanzania kushiriki katika wimbi lijalo la ubunifu wa kiteknolojia nchini.

“Wanawake wanapopewa fursa, hawashiriki tu, bali wanaongoza. Kizazi kijacho cha viongozi katika teknolojia tayari kipo,” alisema.

Alisisitiza zaidi dhamira ya Benki ya Absa Tanzania ya kuweka mazingira jumuishi yatakayowawezesha wanawake kushiriki na kuendelea katika sekta ya teknolojia, sambamba na Lengo la benki hiyo linayosema, “Kuiwezesha Afrika ya Kesho, Pamoja, Hatua Moja baada ya Nyingine", pamoja na ujumbe wa chapa yake usemao "Stori yako ina Thamani".

“Matukio kama haya hayahusu coding pekee; yanahusu kujenga njia za fursa. Tunabaini vipaji, tunakuza uwezo na kufungua milango ya fursa. Benki ya Absa Tanzania imejizatiti kuhakikisha kuwa wanawake vijana walioshiriki hapa wanapata fursa kama mafunzo kwa vitendo, ushauri elekezi na ajira za baadaye,” alisema.

Akizungumza na washiriki ambao hawakupata tuzo, Bw. Mwamfwagasi aliwahimiza kuendelea kuzingatia maendeleo ya ujuzi wao na kuendeleza mawazo yao.

“Kila mtaalamu mkubwa wa teknolojia amewahi kukumbana na changamoto na kushindwa katika baadhi ya hatua. Kinachojali ni namna unavyoitikia changamoto hizo. Chukueni yale mliyojifunza hapa na endeleeni kujenga, kuota ndoto na kusukuma mipaka ya ubunifu,” aliongeza.

Akizungumza kwa niaba ya timu iliyoibuka na ushindi wa jumla, iliyoitwa 'Team Rafikis', Bi. Lilian Msaki, mhitimu wa Uhandisi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Dalaam (DIT), aliishukuru Benki ya Absa na GirlCode Africa kwa kuandaa programu hiyo.

Alisema shindano hilo limemsaidia kuongeza kujiamini katika kutumia teknolojia kubuni na kuendeleza suluhisho za changamoto mbalimbali.

“Ningependa kuwahimiza wanawake wote wenye mawazo ya ubunifu wasiogope kujitokeza. Mnaweza kutatua changamoto nyingi kupitia teknolojia,” alisema Bi. Lilian.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Teknolojia wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Emanuel Mwinuka, alisema mipango kama GirlCode Hackathon inaweza kusaidia kukabiliana na pengo la kijinsia miongoni mwa wataalamu wa mifumo ya kompyuta nchini Tanzania.

“Changamoto hii haipo kwenye sekta ya benki pekee, bali pia katika sekta nyingine. Ndiyo maana sisi Absa tumeamua kuwahamasisha wanawake vijana kutoka vyuo vikuu na sehemu za kazi kutumia fursa zilizopo katika teknolojia na kutumia teknolojia kutengeneza suluhisho mbalimbali,” alisema.

Bw. Mwinuka aliitaja GirlCode Hackathon ya mwaka 2026 kuwa yenye mafanikio makubwa, akibainisha kuwa washindi watapata fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika shindano pana la kimataifa litakalowakutanisha washindi kutoka nchi nyingine zinazoshiriki.

“Hafla ya leo imefanikiwa sana. Tumepata washindi watatu. Kwa kuwa tukio hili linafanyika pia katika nchi nyingine, mshindi wa nafasi ya kwanza atapata fursa ya kushindana na washindi kutoka mataifa mengine kupitia suluhisho walizobuni, ambapo suluhisho bora zaidi litapata tuzo nyingine,” alisema.

GirlCode Hackathon 2026 ilihitimishwa kwa hafla ya utoaji tuzo pamoja na vipindi vya kujenga mahusiano, huku waandaaji na washiriki wakisisitiza kuendelea na juhudi za kuongeza ushiriki na nafasi za uongozi kwa wanawake katika sekta ya teknolojia nchini Tanzania.

Team Rafikis iliibuka mshindi wa jumla, ikifuatiwa na Bizlift katika nafasi ya pili na Nexora ilishinda nafasi ya tatu.
Mkuu wa Mafunzo wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Doris Kibassa (wa tano kutoka kushoto), akikabidhi cheti kwa washiriki wa Timu ya Rafikis, walioibuka kidedea katika shindano la GirlCode Hackathon, wakati wa hafla ya ufungaji rasmi wa mashindano hayo jijini Dar es Salaam jana. GirlCode Hackathon ni sehemu ya mpango mpana wa GirlCode unaotekelezwa barani Afrika kwa lengo la kuwawezesha wanawake vijana kupata ujuzi wa vitendo katika teknolojia, ushauri elekezi pamoja na fursa za kuunda suluhisho zinazolenga kukabiliana na changamoto halisi katika jamii zao. Wengine pichani ni wawakilishi kutoka Benki ya Absa na washirika wa programu hiyo.
Mkurugenzi wa Teknolojia wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Emanuel Mwinuka (kushoto), akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji rasmi wa GirlCode Hackathon 2026, jijini Dar es Salaam jana.
Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Oscar Mwamfwagasi (kushoto), akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake Meneja wa Miradi ya benki hiyo, Bi. Munira Chambuso, wakati wa hafla ufungaji rasmi wa toleo la mwaka huu la GirlCode Hackathon, jijini Dar es Salaam jana. Anayeangalia ni Mkurugenzi wa Teknolojia wa benki hiyo, Bw. Emanuel Mwinuka.
Washiriki wa Absa GirlCode Hackathon 2026, wakipiga picha ya pamoja wakati wa hafla ya ufungaji rasmi wa programu hiyo jijini Dar es Salaam jana.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages