TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) na Shirika lisilo la Kiserikali la Children in Crossfire zimesaini hati ya makubaliano (MoU) kwa lengo la kuimarisha elimu ya awali na elimu ya msingi, hususan katika madarasa ya kwanza na ya pili, kwa kuboresha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa watoto.
Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha uandaaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, kutoa mafunzo kwa walimu na kuimarisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu za elimu katika shule, ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji na kuongeza uwezo wa watoto kumudu stadi za msingi.
Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo imefanyika Oktoba 28, 2026, katika ofisi za TET Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kurasimisha ushirikiano ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka kadhaa kati ya taasisi hizo katika kuboresha elimu ya watoto.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba, amesema makubaliano hayo yamekuja wakati mwafaka, wakati Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na taasisi hiyo ikiendelea kutekeleza mpango mkakati wa kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Amesema kupitia makubaliano hayo, taasisi hizo zitashirikiana kuimarisha uandaaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, miongozo ya walimu pamoja na mafunzo yatakayowawezesha walimu kutekeleza mtaala kwa ufanisi zaidi.


“Tunatarajia kupitia makubaliano haya tutaimarisha uandaaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, pamoja na miongozo ya walimu. Pia, tutaimarisha utoaji wa mafunzo ili kuwawezesha walimu wetu kutekeleza mtaala kwa umakini zaidi,” amesema Dkt. Komba.
Amesema ushirikiano huo pia utasaidia kuwajengea walimu uwezo wa kuandaa madarasa yanayochochea ushiriki wa watoto katika mchakato wa kujifunza, badala ya kutegemea zaidi mbinu za kawaida za ufundishaji.
Dkt. Komba, amesema kuwa Children in Crossfire ina uzoefu katika kuandaa vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinavyosaidia kujenga mazingira ya darasa shirikishi, yanayomwezesha mtoto kushiriki kikamilifu na kufurahia kujifunza.


“Tunatarajia kushirikiana nao kujenga ujuzi huo na kuusambaza kwa walimu wetu ili waweze kuandaa madarasa yanayomfanya mtoto afurahie kujifunza, apende kukaa darasani, na zaidi ya yote, aweze kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Children in Crossfire Tanzania, Craig Ferla, amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano uliokuwepo kwa miaka kadhaa kati ya shirika hilo na TET katika kutekeleza shughuli za kuboresha elimu.
Amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana na TET katika uandaaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, mafunzo kwa walimu na ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu za elimu ya awali shuleni.

“Leo ni siku muhimu kwa shirika letu kwa sababu tumeingia katika makubaliano rasmi na Taasisi ya Elimu Tanzania. Tumekuwa tukishirikiana kwa miaka kadhaa katika kuandaa vifaa vya kufundishia, kutoa mafunzo kwa walimu na kufuatilia utekelezaji wa programu za elimu ya awali,” amesema Ferla.
Ameeleza kuwa kufanikiwa kwa ushirikiano huo kutawezesha shirika hilo kuendelea kutekeleza miradi yake kupitia mifumo na rasilimali zilizopo katika sekta ya elimu nchini, kwa kuzingatia mazingira na muktadha wa elimu Tanzania.
Ferla amesema elimu ya awali na madarasa ya kwanza na ya pili yana umuhimu mkubwa katika safari ya elimu ya mtoto, kwa kuwa ni hatua ambazo hujenga msingi wa utayari wa shule na uwezo wa kumudu stadi muhimu za kujifunza.
Amesisitiza kuwa uwekezaji katika hatua hizo za mwanzo za elimu utasaidia watoto wengi zaidi kupata msingi imara wa kusoma, kuandika na kuhesabu, jambo litakalowawezesha kufanya vizuri zaidi wanapoendelea na elimu ya msingi na hatua nyingine za masomo.
Amesema kuimarishwa kwa msingi huo kutachangia pia kujenga rasilimali watu yenye maarifa na ujuzi unaohitajika katika kukuza uchumi wa Tanzania na kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
Kufikiwa kwa makubaliano hayo kunatarajiwa kuimarisha uratibu kati ya TET na Children in Crossfire, kupanua uwezo wa walimu katika kutumia mbinu bora za ufundishaji na kujenga mazingira yanayowawezesha watoto kupata stadi za msingi katika hatua za mwanzo za elimu yelimu yao.




No comments:
Post a Comment