CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Rabo Foundation imezindua rasmi mradi wa iMBEJU Kilimo Sasa unaolenga kuwawezesha wakulima wadogo 9,000 katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Kagera kupitia upatikanaji wa mitaji, mafunzo ya kilimo cha kisasa, elimu ya fedha, huduma za bima na masoko.
Mradi huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili unalenga kuongeza uzalishaji wa mazao kwa asilimia 30 na kuinua kipato cha kaya za wakulima wanufaika kwa asilimia 25, hatua inayotarajiwa kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na kuboresha maisha ya wakulima.
Akizindua mradi huo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amezipongeza CRDB Bank Foundation na Rabo Foundation kwa kuunga mkono utekelezaji wa Ajenda ya Kilimo 10/30 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amewahimiza vijana nchini kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo biashara, akisisitiza umuhimu wa kushiriki katika shughuli za kilimo zinazotumia teknolojia na mbinu za kisasa ili kuongeza tija na ushindani.
Sambamba na uzinduzi wa mradi huo, CRDB Bank Foundation na Wizara ya Kilimo zimesaini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano kupitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT), inayochangia utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kuwawezesha vijana milioni 10 kushiriki katika mnyororo wa thamani wa kilimo ifikapo mwaka 2030.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema mradi wa iMBEJU Kilimo Sasa unalenga kuwawezesha wakulima wadogo kuachana na kilimo cha kujikimu na kuingia katika kilimo biashara chenye tija na manufaa makubwa kiuchumi.
Amesema msisitizo utawekwa katika matumizi ya mbinu za kilimo himilivu ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuongeza uzalishaji na kujenga ustahimilivu wa shughuli zao za kilimo.
Aidha, mradi huo utawafungulia wakulima fursa mpya za kuongeza kipato kupitia masoko ya kaboni, sambamba na kuwaunganisha na huduma za kifedha na masoko yatakayowawezesha kukuza shughuli zao za kilimo.
Kupitia programu ya iMBEJU Kilimo, CRDB Bank Foundation tayari imewawezesha zaidi ya wakulima wadogo 36,000 kwa kutoa mitaji wezeshi yenye thamani ya shilingi bilioni 5.3, huku juhudi hizo zikichangia uzalishaji wa zaidi ya ajira 10,000 nchini.
Uzinduzi wa iMBEJU Kilimo Sasa unaashiria hatua nyingine katika juhudi za kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima wadogo, kukuza kilimo biashara na kuendeleza mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo nchini.
No comments:
Post a Comment