
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mlezi mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amewataka viongozi wa chama hicho kuachana na vitendo vya kuunda makundi, migogoro na mivutano inayoweza kudhoofisha umoja, mshikamano na misingi ya chama hicho.
Akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani katika Ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, iliyopo Kwa Mfipa, Kibaha, Mhe. Abdulla amesema amekuja kukilea chama kwa ujumla wake bila kujihusisha na makundi yoyote ndani ya chama.
Amesisitiza kuwa CCM ni chama kilicho madarakani na kinachoungwa mkono na wananchi, hivyo viongozi wake wanapaswa kutanguliza umoja na mshikamano badala ya kujihusisha na migogoro inayoweza kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya chama.
"Chama chetu ni chama kilicho madarakani na kinapendwa sana na wananchi, lakini hakiwezi kujengwa kwa makundi wala mivutano," amesema Mhe. Abdulla.
Aidha, amewataka viongozi wote kufanya kazi kwa ushirikiano, kuheshimiana na kuzingatia Katiba, Kanuni na miongozo ya CCM katika kusimamia na kutekeleza shughuli za chama.
Ameeleza kuwa hakuna sababu ya viongozi kuvutana au kujenga uhasama baina yao, akionya kuwa migogoro na mivutano ni kama sumu inayoweza kudhoofisha chama na kuathiri mshikamano wake.
Katika hatua nyingine, Mhe. Abdulla amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kile alichokieleza kuwa ni juhudi za kurejesha heshima ya CCM pamoja na kuimarisha amani na utulivu nchini.
Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa CCM Mkoa wa Pwani wameahidi kumpa ushirikiano Mlezi huyo mpya na kutekeleza maelekezo aliyoyatoa, wakieleza kuwa dhamira yao ni kuimarisha umoja, mshikamano na uendeshaji wa shughuli za chama katika mkoa huo.
Wor’Out Media – Habari, Biashara na Maendeleo.

No comments:
Post a Comment