TAKUKURU YAREJESHA SH MILIONI 37 KWA KUDHIBITI MAGENDO YA MAFUTA - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Wednesday, November 11, 2026

TAKUKURU YAREJESHA SH MILIONI 37 KWA KUDHIBITI MAGENDO YA MAFUTA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Kinondoni, imefanikiwa kuiingizia Serikali mapato ya shilingi milioni 37,120,799 kupitia udhibiti wa uingizaji wa magendo ya mafuta ya kula katika eneo la Pwani ya Kunduchi, jijini Dar es Salaam.

Fedha hizo zimepatikana baada ya kukamatwa kwa madumu 510 ya mafuta ya kula, kila moja yakiwa na ujazo wa lita 20, yaliyokuwa yakiingizwa nchini bila kufuata taratibu za kisheria, ambapo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wahusika walichukuliwa hatua na kulipa ushuru pamoja na adhabu stahiki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Elizabeth Mokiwa, amesema uchunguzi uliofanyika ulibaini kuwa shehena hiyo haikuwa na nyaraka halali za uingizaji nchini wala uthibitisho wa kulipwa kwa kodi na ushuru.

Amesema hatua za kisheria zilichukuliwa dhidi ya wahusika, wakiwemo mmiliki wa shehena ya mafuta hayo pamoja na mmiliki wa gari lililotumika katika usafirishaji wake, hatua iliyowezesha Serikali kurejeshewa mapato hayo.

TAKUKURU imewataka wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa, magendo na ukwepaji kodi, ikieleza kuwa vitendo hivyo vinasababisha upotevu wa mapato ya Serikali ambayo ni muhimu katika kugharamia miradi na huduma za maendeleo.

Taasisi hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali katika kuzuia mianya ya upotevu wa mapato na kuhakikisha sheria zinafuatwa kwa lengo la kulinda uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages