.jpeg)
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Joel Nanauka, amesema uwekezaji katika michezo unahitaji ushiriki wa sekta zote, huku akiipongeza Benki ya CRDB kwa juhudi zake za kuhamasisha na kuendeleza michezo ya aina mbalimbali nchini.

Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Mjini, ameyasema hayo wakati wa mechi ya kirafiki kati ya timu ya wachezaji waliochaguliwa kutoka kwenye ligi yake ya CRDB Nanauka Cup na timu ya wachezaji wa Benki ya CRDB, ambayo ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo. Mechi hiyo ililenga kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
“Mechi hii imehudhuriwa na makocha wa Ligi Kuu Tanzania Bara na wadau wengine wa michezo. Ni sehemu nzuri kwa vijana wetu kujitangaza na kuonyesha vipaji vyao. Michezo ni moja ya nguzo muhimu za ajira kwa vijana. Jambo la uhakika ni kwamba tuna vipaji vingi sana nchini. Nawashukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha michezo nchini,” amesema Waziri Nanauka.
.jpeg)
Akizungumza baada ya mechi hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, jijini Dar es Salaam, na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Wafanyakazi wa Benki ya CRDB, Timothy Fasha, amesema udhamini wa benki hiyo katika michezo unalenga kuwawezesha vijana kutumia vipaji vyao kujipatia fursa na kujikwamua kiuchumi.
.jpeg)
“Benki ya CRDB inaamini uwekezaji katika vijana ni sehemu muhimu ya kujenga jamii yenye uwezo wa kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa, huku michezo ikiwa miongoni mwa majukwaa yanayoweza kuibua vipaji, kukuza ujuzi na kuwajengea vijana msingi wa kufikia malengo yao. Vijana ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya taifa,” amesema Fasha.
Benki ya CRDB, ambayo pia ni mwandaaji wa CRDB Bank International Marathon, inadhamini mashindano mbalimbali ya michezo nchini, yakiwemo Ligi ya Shirikisho, Ligi Kuu ya Mpira wa Kikapu (Taifa Cup), baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na ligi nyingine nyingi za ngazi mbalimbali.
Miongoni mwa ligi hizo ni CRDB Nanauka Cup, inayowashirikisha maelfu ya vijana na kuwapa fursa ya kuendeleza vipaji vyao na kujipatia kipato halali kupitia michezo.
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment