MKE wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi amesema suala kumkomboa msichana wa Zanzibar ni endelevu na linahitaji ushiriki mkubwa wa jamii kupitia taasisi za umma na binafsi.
Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF), aliyasema hayo kwenye kiwanda cha kuzalishia taulo za kike "Tumaini kit” cha taasisi hiyo kilichopo Mnara wa mbao Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi alipotembelewa na Mgeni wake Mwenyekiti wa Taasisi ya misaada ya “National Police Aid Charity” kutoka Uingereza, bi. Marion Tasker.
Mama Mariam Mwinyi alimueleza mgeni huyo na kumuonesha hatua za uzalishaji wa “Tumaini Kit” kiwandani hapo kupitia mradi wa “Tumaini Initiative” wa “Zanzibar Maisha Bora Foundation” ambao umefanikiwa kuzalisha taulo za kike 20,000 kwa mwaka kwa ajili ya hedhi salama.
Naye bi. Morion amepongeza juhudi za maendeleo na kazi nzuri inayofanywa na “Zanzibar Maisha Bora Foundation” ya kuhakikisha wasichana wa Zanzibar hasa wa vijijini wanakua salama muda wote wanapokuwa kwenye ada zao za kila mwezi.
Bi. Morion ni mwanzilishi wa mradi wa “Tumaini Initiative” na ndio aliewafunza vijana wanaotengeneza taulo za kike za "Tumaini kit” miaka miwili iliyopita yupo nchini kwa nia ya kuangalia maendelo ya uzalishaji wa taulo hizo.
Lengo la mradi wa “Tumaini Initiative” ni kutatua changamoto za hedhi kwa wanafunzi wa kike zinazorudisha nyuma maendeleo yao ya Elimu kwa Unguja na Pemba.
Aidha, zoezi la ugawaji wa taulo hizo kwa wanafunzi na wasichana kwa mikoa yote ya Zanzibar ni endelevu ili kuondosha changamooto inayowakumba wasichana wengi wanaoshindwa kuhudhuria vyema kwenye masomo yao wakiwa kwenye ada zao za kila mwezi kwa kukosa taulo za kike na umasikini wa hedhi salama.
Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) iliasisiwa Julai mwaka 2021 na kuzinduliwa rasmi Febuari mwaka 2022.
Mwezi Machi mwaka jana “Zanzibar Maisha Bora Foundation” ilizindua Mpango Mkakati wake wa miaka mitatu na mradi wa “Tumaini Initiative” unalenga kuzalisha taulo za kike zaidi ya 20,000 kwa mwaka hadi sasa ZMBF imefanikiwa kusambaza kwa wanafunzi na wasichana waliobaleghe zaidi ya 4700 wa skuli za msingi na sekondari kwa Unguja na Pemba.
“Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) inafanya kazi kwa karibu na tasisi za Serikali zikiwemo Mahakama ya Zanzibar, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Uchumi wa Buluu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Wazee na watoto, Wizara ya Habari na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.
No comments:
Post a Comment