Wanaharakati na Watetezi wa Maradhi Yasiyoambukiza Wakutana - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Monday, September 30, 2024

Wanaharakati na Watetezi wa Maradhi Yasiyoambukiza Wakutana

Afisa Kutoka Jumuiya ya kuwaendeleza Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Zanzibar Fatma Mwinyiwesa Idarous akielezea jinsi ya namna bora ya ulaji wa matunda na mboga mboga ambao hausababishi madhara kwa binaadamu kwa wanaharakati, watetezi wa maradhi yasiyoambukiza kutoka Jumuiya na vitengo mbali mbali vya serikali na binafsi (hawapo pichani) (kushoto) ni Katibu wa Jumuiya ya Muungano wa Watu wanaoishi na Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar, Omar Abdalla Ali huko katika Jumuiya hiyo Kwa Binti Hamrani Mpendae.
Msaidizi Meneja kitengo cha Maradhi Yasiyoambukiza Wizara ya Afya Zanzibar Zuhura Saleh Amour akitoa ufafanuzi juu ya mikakati ya Serikali kuhusiana na maradhi yasioambukiza kwa wanaharakati, watetezi wa maradhi hayo kutoka Jumuiya na vitengo mbali mbali vya serikali na binafsi (hawapo pichani) (kushoto) ni Mwenyekiti wa Bodi ya Maradhi Yasioambukiza Zanzibar Dk.Said Gharib Bilali, huko katika Jumuiya ya Muungano wa Watu wanaoishi na Maradhi yasiyoambukiza Kwa Binti Hamrani, Mpendae.
Mwalimu wa mazoezi Haji Abdalla Ameir(Colo) akielezea jinsi ya mazoezi yanavyosaidia kuimarisha Afya ya mwili na muitikio uliyopo kwa jamii kwa kuhamasika kufanya mazoezi ili kuepukana na vichocheo vya maradhi yasiyoambukiza Kwa Wanaharakati, watetezi wa maradhi yasioambukiza (hawapo pichani) katika Ofisi ya Jumuiya ya Muungano wa Watu wanaoishi na Maradhi yasiyoambukiza kwa binti Hamdani, Mpendae.
Baadhi ya Wanaharakati Watetezi wa maradhi yasiyoambukiza kutoka Jumuiya na vitengo mbali mbali vya Serikali na binafsi wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Maradhi yasioambukiza Zanzibar Dk.Said Gharib Bilal. (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano wa kubadilisha uzoefu kwa wanaharakati hao katika Jumuiya ya Muungano wa Watu wanaoishi na Maradhi yasiyoambukiza Kwa Binti Hamrani Mpendae.

Na Khadija Khamis, Zanzibar

Msaidizi wa Meneja Kitengo cha Maradhi Yasioambukiza Wizara ya Afya Zanzibar Zuhura Salehe Amour amesema maradhi yasioambukiza bado ni tishio Zanzibar kwa kuathiri na kupoteza viungo vya wagonjwa jambo ambalo linachangia kupoteza nguvu kazi wa taifa.

Hayo ameyasema huko katika ukumbi wa Muungano wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Maradhi Yasioambukiza, Kwa Binti Hamrani wakati wa mkutano wa wanaharakati na watetezi wa maradhi hayo.

Amesema kutokana na ongezeko kubwa la maradhi hayo hivyo iko haja ya jamii kufuata elimu inayotolewa kwa njia mbali mbali ili kuthibiti ongezeko na vichocheo vya maradhi hayo.

Amesema Rais wa Zanzibar Mhe., Dkt. Hussein Mwinyi ameanzisha mpango maalum kuhakikisha anazishughulikia saratani za aina tatu ambazo zinawapa matatizo zaidi kwa akinamama na akinababa ambazo zinaitwa Reproductive Cancer.

Amesema kuwa saratani hizo ni Saratani ya matiti, Shingo ya kizazi na Tenzi dume kwa kufanyika zoezi maalum la uchunguzi wa maradhi hayo katika wilaya mbali mbali kushirikiana na wataalamu kutoka ocean road na hupatiwa tiba mgando kwa wale ambao wanaogundulika na maradhi hayo.

Aidha amesema wizara imejipanga kufikia malengo kwa kutoa elimu zaidi kwa jamii kwa kushirikiana na jumuiya zisizo za serikali pamoja na mashirika mbali mbali ili kuthibiti maradhi hayo.

Sambamba na hayo Serikali kwa kuliona hilo imejipanga kujenga Jengo kubwa la Hospitali ya Saratani ili tiba zote za Saratani zipatikane katika sehemu hiyo.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar (NCDA) Dkt Said Gharib Bilali akifungua mkutano huo kwa Wanaharakati watetezi na ushawishi wa maradhi hayo amewataka kufikisha elimu sahihi kwa jamii juu ya vichocheo vya maradhi na mikakati ya kupambana nayo.

Iwapo jamii itaepuka vichocheo vya maradhi hayo ambavyo ni visababishi kwa kufuata maelekezo ya wataalamu na elimu zinazotolewa na wadau itasaidia kupunguza engezeko la maradhi hayo kwa kiasi kikubwa."

Kwa upande wa Kocha Haji Abdalla Ameir (Colo) amesema amefurahishwa na muitiko mkubwa wa jamii kwa kufanya mazoezi ya viungo jambo ambalo linasaidia kujiepusha na maradhi yasioambukiza kwa kupunguza uzito wa miili yao.

Amesema kuwa zaidi ya watu elfu nne hadi tano hushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Mazoezi Kitaifa kila ifikapo January mosi ya kila mwaka kutoka vilabu mbali mbali vya Unguja na Pemba pamoja na Dar-es-Salam jambo ambalo linaonyesha hamasa iliopo katika jamii.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages