Benki ya Maendeleo
ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Mfuko wa Kukuza Sekta ya Fedha
(FSDT) imewakutanisha pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali za maendeleo nchini
kujadili masuala mbalimbali yatakayosaidia uwekezaji mkubwa katika sekta ya
kilimo Tanzania.
Akizungumza katika
kikao kazi hicho mwenyekiti wa Kikundi Kazi, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo, Bw. Peniel Lyimo alisema kuna haja ya dhamira ya dhati na
uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo nchini ili kusaidia juhudi za Serikali
za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Lyimo alisema kuwa
ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo
nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha
kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa hali inayorudisha nyuma
mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini.
“Kuna haja ya kutafuta suluhisho la changamoto za
upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya Kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya
Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji
wa uchumi na kupunguza umaskini,” alisema.
Akizungumzia
umuhimu wa kikao kazi hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Francis Assenga
alisema kikao hicho kinalenga kuwaleta wadau kutoka sekta mbalimbali ili
kujadili kwa kina njia sahihi za kuchagiza uwekezaji wenye tija katika kilimo
nchini.
Bw. Assenga alisema
kuwa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo kutachagiza kusaidia
uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Kilimo, na kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
“Kimsingi Kikao hiki kinalenga kuanzisha mtandao mpana wa
majadiliano na wadau mbalimbali, zikiwemo Wizara zinazohusika na Kilimo na
Taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi, ili kukubaliana vipaumbele na namna
ya kushirikiana katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya TADB katika kuleta
mapinduzi ya kilimo nchini,” alisema.
Kwa upande wake,
Mkuu wa Kilimo na Fedha Vijijini wa FSDT, Bw. Mwombeki Baregu alisema kuwa FSDT
inalenga kushirikiana na wadau ili kuchagiza ushirikishaji mpana wa washirika
mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili kuongeza uwekezaji katika sekta ya
kilimo nchini.
“Miongoni mwa vikwazo katika kufikia ushirikishwaji wa
fedha nchini Tanzania hasa katika uwekezaji katika kilimo ni pamoja na ukosefu
wa miundombinu sahihi ya soko na upatikanaji wa fedha na huduma na bidhaa zake
maalum katika kilimo, hivyo tunaamini kwa kushirikiana na wadau tunaweza
kutatua changamoto hizi,” alisema Baregu.
No comments:
Post a Comment