Kamati
ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania au Kamati ya Saa 72, ilifanya kikao
chake juzi Ijumaa Aprili 7, 2017 jijini Dar es Salaam na kufikia uamuzi
ufuatao.
Kuhusu kupulizwa dawa
vyumbani Uwanja wa Kambarage:
Daktari
wa Uwanja wa Kambarage, Dk. Abel Kimuntu amekataa kuwasilisha taarifa yake
kuhusu tuhuma za kupuliziwa dawa kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha timu
ya Majimaji katika mechi namba 170 ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya wenyeji
Stand United. Klabu ya Majimaji iliwasilisha malalamiko yake kwa Bodi ya Ligi
kuhusu suala hilo.
Hivyo,
Kamati imeagiza suala la daktari huyo lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya hatua za kinidhamu
dhidi yake kutokana na kukataa kutoa ushirikiano kwa mwendeshaji wa Ligi juu ya
jambo hilo. Kamati ya Nidhamu inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo.
Kuhusu Mchezaji Abdi Banda:
Mechi
namba 194 (Kagera Sugar 2 vs Simba 1). Beki wa Simba, Abdi Banda jezi namba 24
amesimamishwa kucheza Ligi Kuu wakati akisubiri suala lake la kumpiga ngumi
kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla jezi namba 15 wakati akiwa hana mpira
kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF).
Alifanya
kitendo hicho ambacho hakikuonwa na waamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika
Aprili 2, 2017 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Uamuzi wa Kamati
umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.
Pia
Kamati ilibaini kuwa Banda alifanya kitendo cha aina hiyo kwenye mechi namba
169 kati ya Simba na Yanga iliyofanyika Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Awali,
Klabu ya Kagera Sugar iliwasilisha malalamiko dhidi ya kitendo cha beki wa
Simba, Abdi Banda kumpiga ngumi kiungo wao George Kavilla wakati akiwa hana
mpira, na Mwamuzi wa mechi hiyo kutochukua hatua yoyote.
Kwa
vile kosa hilo ni la kinidhamu, Kamati imemsimamisha Abdi Banda kwa mujibu wa
Kanuni ya 9(5) wakati akisubiri suala lake kusikilizwa na kutolewa uamuzi na
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Kamati ya
Nidhamu inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo.
Kadhalika
Klabu ya Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na
mabao matatu kutokana na timu ya Kagera Sugar kumchezesha mchezaji Mohamed
Fakhi Gharib wakati akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194
iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kamati
baada ya kupitia malalamiko hayo, imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili
13, 2017 kwa vile bado inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo
kabla ya kufanya uamuzi.
Mechi
namba 195 (Yanga 1 vs Azam 0). Yanga haikuingia kwenye chumba chake cha
kubadilishia nguo, kutokana na kuwa na maji yaliyomwagwa na wanachama wa klabu
hiyo (makomandoo) muda mfupi kabla ya timu hiyo kuwasili uwanjani.
Kamati
imeelekeza klabu ya Yanga iandikiwe barua ya onyo, na kuitaka kuhakikisha
wanachama wake wanaacha mara moja mtindo wa kumwaga maji vyumbani baada ya kuwa
vimeshafanyiwa usafi na wafanyakazi wa uwanja tayari kwa ajili ya matumizi ya
timu yao.
Mechi
namba 200 (Majimaji 4 vs Toto Africans 1). Katika mechi hiyo, timu ya Toto
Africans ilifanyiwa vurugu ikiwa njiani kurejea hotelini baada ya mechi hiyo
ambapo viongozi wake wawili waliumizwa. Tukio hilo liliripotiwa Kituo cha
Polisi, na kesi tayari iko kortini.
Kituo
cha Songea (Uwanja wa Majimaji) kiandikiwe barua ya kuhakikisha hazitokei
vurugu uwanjani hapo baada ya mechi ikiwemo kuhakikisha timu ngeni inatoka
uwanjani salama hadi kwenye hoteli ilikofikia. Iwapo vurugu zitaendelea, Bodi
ya Ligi itasimamisha matumizi ya kituo hicho kama ilivyoainishwa katika Kanuni
ya 9(2) ya Ligi Kuu.
KUPITIA MATUKIO YA LIGI
DARAJA LA PILI (SDL Play Off)
Mechi
namba 7 (Mawenzi Market 2 vs Transit Camp 0). Klabu ya Transit Camp imepigwa
faini ya sh. 200,000 (laki mbili) baada ya timu yake kuchelewa uwanjani kwa
dakika 45 katika mechi hiyo iliyochezwa Machi 18, 2017 katika Uwanja wa Jamhuri
mjini Morogoro. Adhabu dhidi ya Transit Camp imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya
14(1) na 14(47) kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kocha
Msaidizi wa Transit Camp, Thomas Gama amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya
sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutolewa nje na Mwamuzi katika mchezo kutokana
na kumtolea maneno ya kashfa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja.
Mechi
namba 8 (JKT Oljoro 1 vs Cosmopolitan 0). Klabu ya Cosmopolitan iliwasilisha
malalamiko kuwa mechi hiyo iliyofanyika Machi 20, 2017 kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha ilichezeshwa na Mwamuzi wa
Arusha, badala ya Mwamuzi kutoka Singida aliyekuwa amepangwa awali.
Kamati
imetupa malalamiko hayo kwa vile si ya kweli, na Mwamuzi aliyechezesha mechi
hiyo alitoka Mkoa wa Manyara, na si Arusha kama walivyodai katika malalamiko
yao.
Mechi
namba 12 (Transit Camp 1 vs Cosmopolitan 1). Daktari wa Cosmopolitan, Najim
Mtoro amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada
ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kumtukana Mwamuzi wa Akiba.
No comments:
Post a Comment