Daktari bingwa kutoka Jamhuri ya Watu wa China Dk. Gao, akimpima kifua mtoto
Salma Mohammed mkazi wa Kilmahewa, katika siku ya Afya ya Kijiji iliyofanyika
Shule ya Kwamtipura Wilaya ya Mjini Unguja.
Daktari bingwa wa pua na masikio kutoka China Dk. Fei Jie, akimfanyia
uchunguzi wa pua Bi. Amina Himid katika siku ya Afya ya kijiji iliyofanyika
Shule ya Kwamtipura.
Afisa Afya akimpatia dawa mmoja wa wagonjwa waliofika kupata huduma
katika siku ya afya ya kijiji huko Skuli ya Kwamtipura Wilaya ya Mjini.
Vijana wakiwa kwenye
foleni wakisubiri kuonana na daktari kwa ajili ya uchunguzi.
Wananchi waliojitikeza kupatiwa huduma katika siku ya Afya ya Kijiji
huko Skuli ya Kwamtipura.
Watoto wakinywa Uji mara baada ya kupatiwa huduma za afya.
Mkurugenzi wa Kinga na
elimu ya afya Dk. Fadhil Mohammed Abdalla, amewataka wananchi wajitokeze kwa
wingi kupima afya zao.
Amesema hatua hiyo ni
muhimu kwani humuwezesha mtu kubaini mapema iwapo amepata maradhi na hivyo
kutibiwa kabla athari haijwa kubwa.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo wakati wa kutolewa huduma za afya katika shehia ya Kilimahewa
Bondeni kutoka kwa madaktari bingwa wa China, amesema kuwa ni vyema kunapotokea
fursa ya huduma bila malipo, wananchi wazichangamkie ipasavyo.
Dk. Fadhil alisema
serikali imekuwa ikichukua juhudi kubwa kuwafikishia wananchi huduma za afya
karibu na maeneo yao wanakoishi.
“Huduma hii adhimu na ni
muhimu kwa kujua afya yako na baada ya kupata vipimo unapata matibabu na
wengine hushauriwa wafike hospitali ya Mnazi mmoja kwa kupata matibabu zaidi.”
Alisema mkurugenzi huyo.
Dk. Fadhil amesema lengo
la huduma hizo ni kuwashajiisha wananchi waweze kuelewa maradhi waliyonayo na
kuwezesha kupatiwa matibabu.
Aidha alieleza kuwa,
madaktari hao hutoa elimu ya afya kuhisiana na maradhi ya kuambukiza hasa
katika kipindi hichi cha mvua.
Nae daktari dhamana wa
wilaya ya mjini Ramadhani Mikidadi Suleiman, amesema zoezi la kupima afya ni
muhimu na wataalamu wa kutosha wapo hivyo wananchi wasipuuze kujitokeza.
Katika uchunguzi
uliofanya kweny zoezi hilo, Dk. Mikidadi alisema wananchi wengi wamegundulika
na matatizo ya macho, meno, koo, kisukari na shinikizo la damu na kupatiwa
matibabu.
Amewahimiza wananchi
kutodharau zoezi hilo litakalokuwa linafanyika kila baada ya miezi mitatu.
Naye sheha wa shehia ya
Kwamtipura Hassan Hashir Hassan, ameeleza kufurahika kwake kutokana na wananchi
wengi kuitikia wito na kujitokeza katika zoezi hilo lililofanyika bila ya
malipo.
Maradhi mengine
yaliyogunduliwa kutokana na uchunguzi ni tezi dume, maradhi ya mama na mtoto
pamoja na kuchukuliwa vipimo vya maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Wananchi mbalimbali
wameipongeza serikali kwa kuwafikishia huduma hizo katika maeneo yao,
wakisema imesaidia kuwapunguzia usumbufu na gharama za kwenda mbali.
No comments:
Post a Comment