Kulikuwa na
mfalme mmoja aliyekuwa na mbwa kumi wakali sana. Alipenda kuwatumia mbwa hawa
pindi akitaka kumuadhibu mtumwa aliyekosea. Mbwa hawa waliwatesa watumwa kwa kuwararua na meno yao makali! Wakati
mwingine watumwa waliokutana na adhabu hii walipoteza uhai.
Siku moja
mtumwa aliyemtumikia mfalme kwa miaka kumi alitoa wazo baya ambalo
halikumpendeza mfalme, ikaamriwa akamatwe na kutupwa katika banda la mbwa. Mtumwa
alinung'unika na kusema :"nimekutumikia kwa miaka 10, na leo wanitenda
hivi? Naomba unipe walau siku 10 kabla hujanitupa bandani! " Mfalme
akakubali.
Katika siku
hizo 10, mtumwa alimfuata mlinzi wa banda la mbwa na kumuomba ampe nafasi ya
kuwahudumia mbwa wale. Mlinzi alistaajabu ila akakubali. Mara moja mtumwa
akaanza kazi ya kuwapa mbwa chakula, kuwaogesha na kila aina ya faraja ambazo
wanyama huhitaji.
Siku 10
zikaisha, mfalme akaamuru mtumwa atupwe bandani kutumikia adhabu yake. Hilo
likafanyika kwa haraka, lakini cha kushangaza mbwa walianza kulamba miguu ya
mtumwa na si kumrarua kama ilivyotegemewa.
Mfalme
akastaajabu, akasema:"Nini kimewasibu mbwa wangu?" Mtumwa akajibu "nimewahudumia
mbwa hawa kwa siku 10 tu na hawajasahau fadhila zangu. Lakini kwa upande wako nimekutumikia miaka 10, hata hivyo umesahau yote kwa
sababu ya kosa moja tu! "
Kufikia hapo
mfalme akatambua kosa lake na akaamuru mtumwa aachiwe huru.
Katika maisha
kuna watu husahau mambo mema waliyotendewa na wengine pindi wakikosewa.
Kamwe
usiruhusu historia nzuri kufutika sababu ya jambo moja usilolipenda! Tembea
katika msamaha kila wakati.
Mungu
Awabariki wote.
No comments:
Post a Comment