Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta akimkabidhi ya vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya usikilizaji wa mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao.
Picha ya pamoja ya viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma na uongozi wa gereza la Kibondo.
Na Festo Sanga- Mahakama, Kigoma
Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Kigoma, imefanikiwa kusikiliza mashauri kwa asilimia 77 baada ya kujiwekea malengo ili hakikisha haki inatolewa kwa wakati tofauti na Mkakati wa Mahakama ya Tanzania.
Akizungumzia kuhusu suala hilo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Ilvin Mugeta alisema kanda hiyo ina mpango iliyojiwekea wa muda wa usikilizaji wa mashauri.
‘‘Mpango huu unalenga kusimamia utoaji haki kwa haraka katika viwango vya kanda tulivyojiwekea ambapo Mahakama za Mwanzo kesi itadumu kwa (miezi mitatu), Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi zitadumu (miezi minne) na Mahakama Kuu (miezi sita), akitolea mfano kwa upande wa Mahakama Kuu kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu walipokea mashauri 190 na yaliyomalizika ni mashauri 165 sawa na asilimia 77,’’ alisema Jaji Mugeta.
Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano (2015/16 hadi 2019/20), inasisitiza utoaji haki kwa wote na kwa wakati ambapo imejiwekea muda wa kumalizika kwa shauri mahakamani. Katika Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama za wilaya shauri linatakiwa kumalizika ndani ya miezi 12, Mahakama Kuu ndani ya miaka miwili na Mahakama za Mwanzo ni miezi sita.
Jaji Mugeta aliongeza kwamba alifanya ziara katika Wilaya za Kasulu na Kibondo Juni 23 hadi 24 mwaka huu, ambapo alikabidhi kwa Wakuu wa Magereza ya Kasulu na Kibondo vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) ili kuwezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao ‘Video Conference’.
Alivitaja vifaa vilivyokabidhiwa kwenye magereza hayo kuwa ni Televisheni (TV inch 32), kompyuta mpakato (Laptop), Modem zenye laini za simu zenye kifurushi cha GB 34 kwa kila Gereza .
‘‘Vifaa hivyo vya TEHAMA vitapunguza adha ya mahabusu na wafungwa kukosa kufika Mahakamani kutokana na changamoto ya usafiri,’’ alisema Mhe. Mugeta.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji kwa vitendo wa maagizo ya Jaji Mkuu wa Tanzania, kuhusu kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika kusajili na kusikiliza mashauri kwa mtandao.
Aidha, Jaji Mugeta alisema usambazaji wa vifaa hivyo ni utekelezaji dhahiri wa mpango wa ndani wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Kigoma uliozinduliwa rasmi katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria iliyofanyika Februari 6, mwaka huu.
Pamoja na kukabidhi vifaa hivyo, Jaji Mugeta alitembelea pia ofisi za wakuu wa Wilaya za Uvinza, Kakonko, Kibondo, Kasulu na Buhigwe kwa lengo la kuhimiza kamati za maadili za Mahakimu na Maafisa wa mahakama kukutana kwa mujibu wa Muongozo wa Uendendeshaji wa Kamati za Maadili.
Jaji Mugeta katika ziara hiyo aliambatana na Naibu Msajili na Mtendaji wa Mahakama hiyo ambapo walitembelea viwanja vya Mahakama ambavyo vina vinatarajiwa kujengwa Mahakama za Wilaya za Uvinza, Buhigwe na Kakonko.
No comments:
Post a Comment