
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akimsikiliza Mratibu wa Kitengo cha Sema na Rais Mwinyi (SNR) Ikulu Nd,Haji Khamis Makame (kulia) wakati alipofika katika Ofisi ya kitengo kuzungumza na Wafanyakazi na kusikiliza taarifa mbali mbali na changamoto wanazokabiliana nazo wakiwa wanatimiza Mwaka Mmoja tokea kuanzisha kwa kitengo hicho.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akizungumza Wafanyakazi wa kitengo cha Sema na Rais Mwinyi (SNR) Ikulu wakati alipofika katika Ofisi ya kitengo kusikiliza taarifa mbali mbali na changamoto wanazokabiliana nazo wakiwa wanatimiza Mwaka Mmoja tokea kuanzisha kwa kitengo hicho,(kulia) Mkuu wa Kitengo hicho Nd,Haji Khamis Makame. [Picha na Ikulu]
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa Watendaji wa Serikali kuhakikisha wanashughulikia ipasavyo malalamiko yanayowasilishwa na wananchi kupitia Mfumo wa Sema na Rais Mwinyi (SNR) ili mfumo huo uweze kuleta tija na kuwa endelevu.
Dk. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipozungumza na watendaji wa Kitengo cha SNR Ofisi ya Rais Ikulu, ambapo pamoja na mambo mengine alipokea taarifa za kiutendaji kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu mfumo huo uzinduliwe February 27, 2021.
Alisema wasimamizi wa mfumo huo katika taasisi na Wizara za Serikali wanapaswa kuhakikisha Maofisa wanaoshughulikia mfumo huo wanatimiza wajibu wao ipasavyo na kusema Serrikali inakusudia kuimarisha mfumo huo pamoja na kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa umma siku zijazo.
Alisema lengo la Serikali la kuanzisha mfumo huo ni kuwawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko yao Serikalini ili yaweze kutafutiwa njia nzuri ya kuyashughulikia na kuyapatia ufumbuzi.
Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi kuwa mfumo wa SNR umepata mafanikio mazuri na kusema Serikali itaendelea na juhudi za kuzitafutia ufumbuzi changamooto mbali mbali zinazowasilishwa ambazo hadi sasa bado hazijapatiwa ufumbuzi.
Alisema dhamira ya serikali ni kuyapatia ufumbuzi malalamiko yote yanayowasilishwa, hivyo akataka kuwepo mashirikiano kutoka kwa kila mtu.
Dk. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwapongeza Watendaji wa kitengo cha SNR Ofisi ya Rais Ikulu, pamoja na watendaji wa SNR walioko katika Taasisi na Wizara mbali mbali za Serikali kwa kazi nzuri wanayofanya, huku akibainisha malalamiko mengi yakiwa yamefanyiwa kazi.
Alisema katika kipindi hicho asilimia 73 ya malalamiko yaliowasilishwa yamewweza kupatiwa ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment