SERIKALI YA ZANZIBAR YAFUNGUA FURSA KWA VIJANA - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Thursday, March 12, 2026

SERIKALI YA ZANZIBAR YAFUNGUA FURSA KWA VIJANA

Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji Mhe. Shabaan Ali Othman amesema Serikali imeanzisha Wizara hiyo ili kushughulikia changamoto za vijana na kuzipatia ufumbuzi katika suala la ajira, kuwajenga katika moyo wa kizalendo ili kuipenda nchi yao na kudumisha amani na utulivu pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuhusu siku 100 za mafanikio ya uongozi wa awamu ya pili ya Dkt. Mwinyi amesema lengo ni kuwaletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kuviimarisha vyama vya ushirika ili kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Amesema kuwa Serikali imekusudia katika kipindi cha miaka mitano kuimarisha mazingira wezeshi kwa maendeleo ya vijana yakiwemo kuwajengea uwezo wa kazi na kutengeneza nafasi za ajira zisizopungua 350,000 kwa wananchi wote hasa vijana kupitia sekta mbalimbali.

Wizara hii haiajiri ila jukumu lake kubwa ni kuratibu upatikanaji wa fursa hizi za ajira kwa kushirikiana na Sekta nyingine zote za Serikali na Binafsi ili mikakati hii ya Serikali iweze kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa” ameeleza.

Akizungumzia sekta ya uwezeshaji kiuchumi Waziri Shabaan amesema Wizara imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7 kupitia mifuko ya Abu Dhabi na Inuka kwa kuwapatia wananchi 4,867 ambao wamenufaika na mkopo huo ni wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Wizara imetoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa fedha kwa zaidi ya wajasiriamali 600 Unguja na Pemba ambapo mafunzo hayo yamehusisha fani mbalimbali ikiwemo usarifu wa mazao, ufugaji wa nyuki, utengenezaji wa sabuni na bidhaa za urembo pamoja na matumizi ya teknolojia ya nishati ya jua” amefahamisha.

Amesema katika kuimarisha sekta ya ushirika, Wizara imesajili vyama vipya vya ushirika 475 na kufanya ukaguzi wa vyama 271 ili kuhakikisha vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria pamoja na kuwapatia mafunzo viongozi wa vyama vya ushirika ili kuboresha uendeshaji wa miradi na usimamizi wa fedha.

Waziri Shabaan amefafanua kuwa Serikali imepanga mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha vituo vya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi katika wilaya ili kuimarisha mifumo ya kidigitali ya ukusanyaji wa takwimu na kuongeza elimu ya uzalendo kwa vijana.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages