
●Ni juhudi za kahamasisha matumizi ya Nishati Safi.
●Matumizi ya Nishati safi Rafiki Briquettes kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya 1000
●Yafunga mitambo ya kuzalisha tani 20 kwa saa moja.
Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imejipanga kuhakikisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia kupitia mradi wa Rafiki Briquete yanaongezeka katika mikoa mbalimbali nchini ili kufikia asilimia 86 ya matumizi ya Nishati Safi ifikapo mwaka 2030.
Hayo yameelezwa leo Machi 12, 2026 Mkoani Tabora na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipokuwa ikikagua miradi inayosimamiwa na Wizara ya Madini.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, STAMICO tayari imeshanunua Mitambo minne yenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa ambayo imesimikwa katika maeneo ya Kiwira, Pwani, Chigongwe Mkoani Dodoma na Kiloleni Mkoani Tabora.
Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, kwa Mkoa wa Tabora, STAMICO imelenga kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi kwa wakulima wa Tumbaku ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia kuni kwa wingi suala linalohusisha uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Subira Mgalu ameipongeza STAMICO kwa ubunifu wa miradi endelevu yakimkakati inayoleta mchango mkubwa kwa taifa ikiwa pamoja na kuunganisha mnyororo mzima wa thamani madini.
Mgalu ameitaka STAMICO kuanza uzalishaji mapema pamoja na kufungua matawi mengine katika mikoa mbalimbali nchini ili kutekeleza Agenda ya kitaifa inayohusu matumizi ya Nishati Safi ili kufikia asilimia 86 za matumizi ya Nishati Safi ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake Msafiri Mbibo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini , ameishukuru kamati kwa maoni mbalimbali yaliyolenga uboreshaji wa mradi huo hususan katika upande wa ajira na Usimikaji wa mitambo ya Uzalishaji.
Awali, akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo Deusdedith Magala, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, amesema kuwa mradi wa Rafiki Briquettes katika Mikoa mbalimbali unatarajia kuajili watanzania zaidi ya 1000.







No comments:
Post a Comment