
DAR ES SALAAM; Septemba 20, 2026 — Mbuzi wa Benki ya NMB, ‘NMB the GOAT’, ameibuka mshindi katika mashindano ya mbio za mbuzi yaliyopewa jina la ‘NMB unGOATable Race’, yaliyofanyika Septemba 19, 2026, akimshinda mbuzi wa Bowman katika tukio lililolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia elimu ya juu kwa vijana.
Mashindano hayo, maarufu kama Goat Races, yamelenga kuchangisha Sh200 milioni zitakazosaidia vijana 150 wenye changamoto za kifedha kupata fursa ya kuendelea na elimu ya juu.

NMB Bank imeshiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo ikiwa miongoni mwa wadhamini wakuu, huku ushindi wa ‘NMB the GOAT’ ukiongeza mvuto katika ushiriki wa benki hiyo kwenye tukio hilo la kijamii.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki kwa Wateja Maalumu wa NMB, Getrude Mallya, alisema ushindi huo umefanya ushiriki wa kwanza wa benki katika mashindano hayo kuwa wa kipekee.
.jpeg)
Mallya alisema NMB inajivunia kuunga mkono tukio linalounganisha burudani na uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kuwasaidia vijana wanaokabiliwa na changamoto za kifedha katika kuendelea na masomo yao.
“Zaidi ya furaha ya ushindi, ushiriki wetu katika mashindano haya unaakisi dhamira ya Benki ya NMB ya kuunga mkono jitihada zinazofungua fursa kwa vijana wa Kitanzania. Mashindano haya yanatuunganisha kwa lengo muhimu la kuchangisha fedha kusaidia elimu,” alisema Mallya.
.jpeg)
Kwa upande wake, Rais wa Rotary Club ya Dar es Salaam Oysterbay, Paul Muhato, alisema wanafunzi 350 wamewezeshwa kuendelea na masomo tangu klabu hiyo ilipoanza kusimamia rasmi mashindano hayo mwaka 2018.
Alisema mashindano ya mwaka huu yanalenga kuongeza idadi hiyo kwa kuwawezesha wanafunzi wengine 150 kupata elimu ya juu mwaka 2027.
Goat Races zimeendelea kuwa moja ya matukio yanayochanganya burudani, michezo na shughuli za kijamii, huku fedha zinazopatikana kupitia tukio hilo zikilenga kusaidia vijana kupata fursa ya elimu ya juu.
Ushiriki wa NMB katika mashindano hayo unaongeza wigo wa shughuli za benki katika kusaidia programu zinazolenga uwezeshaji wa vijana na maendeleo ya jamii.

.jpeg)
.jpeg)



No comments:
Post a Comment