Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini yapongeza mpango wa iMBEJU Nuru unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi vijijini.
Dar es Salaam, Tanzania; Novemba 23, 2026 – Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepongeza mpango wa CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa kutoa ruzuku ya Shilingi 27,000 kwa kila kaya yenye kipato cha chini vijijini ili kuiwezesha kuunganishiwa huduma ya umeme.
Mpango huo unaotekelezwa kupitia Programu ya iMBEJU Nuru, unalenga kupunguza changamoto za gharama za kuunganishiwa umeme kwa kaya zenye uwezo mdogo wa kiuchumi, huku ukichangia juhudi za Serikali za kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme nchini.
Kamati hiyo imesema mpango huo utasaidia kuharakisha maendeleo ya jamii za vijijini kwa kuwezesha wananchi kupata huduma ya umeme, ambayo ni muhimu katika kuboresha maisha, kuongeza shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi.
Mpango huo unalenga kuwezesha kuunganishiwa umeme kwa kaya 510,000 kila mwaka na ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono Mpango wa Taifa wa Nishati (M300), unaolenga kuunganisha kaya mpya milioni 8.3 na kufikisha kiwango cha upatikanaji wa umeme kwa asilimia 75 ya kaya nchini ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Subira Mgalu, amesema mpango huo utaongeza uhakika wa wananchi kupata huduma ya umeme kupitia utaratibu wa ruzuku na mikopo yenye masharti nafuu kwa wenye uhitaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali kufadhili miradi ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi, kuvutia uwekezaji na kuboresha maisha ya Watanzania.
Amesema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya Benki ya CRDB katika kusaidia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa kupitia upatikanaji wa huduma muhimu na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema kupitia programu ya iMBEJU Nuru, kila kaya ya kijijini yenye kipato cha chini na isiyo na uwezo wa kugharamia gharama za kuunganishiwa umeme itapata ruzuku ya Shilingi 27,000.
Amesema fedha hizo zitalipwa moja kwa moja kwa TANESCO baada ya mnufaika kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme, hatua inayolenga kuhakikisha msaada huo unamfikia mlengwa na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Aidha, Tully amesema kaya hizo zitakuwa na fursa ya kupata mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 10 kwa wateja wa TANESCO watakaohitaji kusambaza umeme katika maeneo mengine ya nyumba zao au kuuwezesha katika miradi yao ya kuwaingizia kipato.
Ameeleza kuwa utaratibu huo utawasaidia wananchi kupata nishati safi na salama majumbani, pamoja na kuongeza uwezo wa kuendesha shughuli za kiuchumi zinazotegemea nishati ya umeme.
Akifafanua utaratibu wa kurejesha mikopo hiyo, Tully amesema marejesho yatafanyika kwa njia rahisi kupitia mfumo wa malipo ya umeme wa LUKU.
“Mkopo huu nafuu utarejeshwa kwa njia rahisi kabisa, mteja atakatwa kila anaponunua LUKU,” amesema Tully.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuharakisha upatikanaji wa nishati nchini.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za wananchi na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kupitia programu ya iMBEJU Nuru, CRDB Bank Foundation na TANESCO wanaendelea kuunga mkono juhudi za kuongeza upatikanaji wa umeme kwa wananchi wenye kipato cha chini, hususan katika maeneo ya vijijini, ili kuhakikisha nishati inakuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
No comments:
Post a Comment