NMB YAFUNGUA MILANGO YA SOKO KWA WABUNIFU VIJANA WA UDSM KUPITIA TEKNOLOJIA - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Tuesday, November 24, 2026

NMB YAFUNGUA MILANGO YA SOKO KWA WABUNIFU VIJANA WA UDSM KUPITIA TEKNOLOJIA

Dar es Salaam - Novemba 24, 2026: Benki ya NMB inaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kukuza vipaji, ubunifu na ujasiriamali miongoni mwa vijana, kwa kuwaunganisha wabunifu na fursa za ushauri wa kitaalamu, ukuzaji wa biashara na upatikanaji wa masoko kupitia teknolojia.
Akizungumza wakati wa maonesho ya bunifu za wanafunzi yaliyojulikana kama NMB–UDSM Innovation Showcase, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Rasilimali Watu na Vitengo vya Biashara wa NMB, Erica Hanson, amesema kupitia NMB Innovation Hub pamoja na ushirikiano na idara mbalimbali za biashara za benki hiyo, wabunifu vijana watapata fursa ya kuboresha bunifu zao na kuendeleza bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya soko.
Amesema ushirikiano huo unalenga kuwasaidia vijana kuvuka hatua ya kuwa na mawazo ya kibunifu na kuyabadilisha kuwa bidhaa na huduma zinazoweza kuingia sokoni, kukua kibiashara na kuwa na mchango katika maendeleo ya uchumi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Utafiti na Ubunifu, Dkt. Cosmas Mushi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya vyuo vikuu na sekta binafsi katika kukuza wataalamu wa teknolojia na kuimarisha mazingira ya ubunifu nchini.

Amesema bunifu zilizowasilishwa katika maonesho hayo zimeendelezwa kwa kipindi cha takribani miezi mitatu, kuanzia hatua ya mawazo hadi kufikia hatua ya kuwa bidhaa zinazoweza kufanyiwa tathmini na kuendelezwa zaidi.

Maonesho hayo pia yalihudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Ubunifu wa NMB, Innocent Shirima, yakionesha namna ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu na sekta ya fedha unavyoweza kusaidia kuunganisha maarifa ya kitaaluma na mahitaji halisi ya soko.

Kupitia ushirikiano huo, NMB na UDSM zinaendelea kuweka mazingira yanayowawezesha vijana kutumia maarifa na ujuzi walioupata darasani kubuni suluhisho za changamoto mbalimbali, kuanzisha biashara, kutengeneza fursa za ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Hatua hiyo inaakisi nafasi ya sekta ya benki katika kusaidia maendeleo ya ubunifu na ujasiriamali wa vijana, huku ikifungua fursa zaidi za kuunganisha bunifu za ndani na mahitaji ya soko la Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages