KESI YA LEMA IMEIBUA MAPINDUZI YA KISHERIA - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Monday, March 6, 2017

KESI YA LEMA IMEIBUA MAPINDUZI YA KISHERIA


Kesi ya tuhuma za uchochezi inayomkabili mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, inaendelea, lakini inaweza kuwa imejenga misingi ya utoaji haki kwa vyombo vya Serikali, mawakili na mahakama.

Lema alipata dhamana Ijumaa baada ya kukaa mahabusu kwa siku 121 kutokana na sarakasi za kisheria baada ya ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kuweka pingamizi dhidi ya dhamana yake alipofikishwa kortini kwa mara ya kwanza.

Akitoa dhamana hiyo, Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kaskazini alisema uamuzi wa Mahakama ya hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha kumpa dhamana Lema, Novemba 11 mwaka jana ulikuwa sahihi na hakukuwa na sababu za kupinga.

Alisema DPP angekuwa na haki ya kupinga dhamana iwapo mshtakiwa asingetimiza masharti ya dhamana na si vinginevyo.

Jaji huyo alizielekeza mahakama za chini kusimamia mamlaka yake bila kuyaachia na kuzitaka ziheshimu misingi ya sheria.

Alikuwa akirejea kitendo cha Hakimu Mkazi wa Arusha kuacha kuendelea na masharti ya dhamana aliyompa Lema baada ya mawakili wa Serikali kumtaarifu kwa mdomo kuwa wana nia ya kukata rufaa kupinga dhamana hiyo.

Tangu wakati huo, dhamana ya Lema ilikuwa ikitegemea sarakasi hizo za kisheria zilizotinga hadi Mahakama ya Rufaa ambayo katika uamuzi wake iliweka bayana kuwepo kwa sintofahamu.

Lakini Februari 28 wakati wa kutoa uamuzi kuhusu pingamizi la dhamana lililowekwa na Serikali, Jaji Bernard Luanda, ambaye aliongoza jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, alionyesha kushangaa jinsi ofisi ya DPP ilivyoshughulikia suala hilo, ikiwa ni pamoja na kuondoa rufaa siku ya uamuzi,

Jaji Luanda alisema tabia ya wanasheria wa DPP inanajisi taaluma na hivyo kuitaka ifanye kazi kwa njia ambayo haitaonea wananchi.

Pia majaji hao walitupa mapingamizi mawili yaliyokuwa yamewasilishwa na ofisi ya DPP.

Kauli ya Jaji Maghimbi na ya majaji hao ni kama zimejenga msingi wa utoaji haki kwa vyombo hivyo.

“Ofisi ya DPP na Mwanasheria Mkuu wa Serikali zilipaswa kuwa ni watetezi wa haki, lakini zimebadilika na sasa zinatumika kukandamiza watu wakose haki zao,” alisema mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche.

“Leo mbunge amekaa miezi minne gerezani kwa kosa ambalo lina dhamana. Tujiulize ni Watanzania wangapi wanasota magereza kutokana na DPP na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushindwa kusimamia sheria?”

Alisema Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia vyakula vya wafungwa, lakini uchunguzi wa kina ukifanyika itabainika wengi wapo jela kutokana na ofisi hizo mbili kutotimiza wajibu wao.

Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hamis Mkindi alisema kosa la kutoa lugha ya uchochezi lina dhamana, lakini kilichokuwa kinafanyika ni ukiukwaji wa sheria.

Mkindi alisema hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi dhamana ni haki ya mtuhumiwa, lakini haki hiyo ilikuwa inachelewa kutokana na DPP kutumia vibaya mamlaka yake.

Mwanasheria wa Chadema, Peter Kibatala alisema tangu kuanza kwa shauri hilo walikuwa wanatetea haki na hadhi ya mahakama ambayo alidai iliporwa na DPP.

Kibatala, ambaye pia ni mmoja wa mawakili wa Lema, alisema wanashukuru kwa uamuzi wa Jaji Maghimbi kutoa dhamana.

“Jaji aliweka wazi kwenye uamuzi wake, mahakama za chini zinatakiwa kuheshimiwa na pia kuzuia DPP kuweka mapingamizi yanayokiuka haki,” alisema.

Mara baada ya Lema kutoka nje kwa dhamana, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema:

“Mhe Lema, karibu sana uraiani. Aliyeshinikiza unyimwe dhamana alidhani anakukomoa, kumbe anazidi kukuimarisha. Hongera sana Kamanda.”

Msanii wa filamu nchini aliyejiunga na Chadema hivi karibuni, Wema Sepetu naye aliandika katika ukurasa wa Instgram akimpongeza Lema na kwenda Arusha kumtembelea.

“Kwenye mapambano haya hautakuwa mwenyewe. Mdogo wako Wema nitakuunga mkono mpaka kieleweke,” aliandika msanii huyo.

Ofisa mmoja wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema ofisi hiyo haipaswi kunyooshewa kidole cha lawama kwa sababu mahakama ilikuwa na uwezo wa kuingilia mapema na kutoa uamuzi inayoona unafaa.

“Hawakuwa na sababu ya kukaa kimya siku zote na kuja kutoa lawama hivi sasa,” alisema ofisa huyo.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages