SERIKALI YAZINDUA MFUMO JUMUISHI WA KIELEKTONIKI WA VIWANGO VYA ZBS VISIWANI ZANZIBAR - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Thursday, February 20, 2025

SERIKALI YAZINDUA MFUMO JUMUISHI WA KIELEKTONIKI WA VIWANGO VYA ZBS VISIWANI ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi mbali mbali, watendaji wa Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) na washiriki mbali mbali kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki wa Viwango wa ZBS (ISQMT)uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwekeza katika Mifumo na Teknolojia za Kisasa ili kuhakikisha usimamizi wa viwango vya bidhaa unafanyika kwa ufanisi zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki (ISQMT) uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.

Amesema kuzinduliwa kwa mfumo Jumuishi wa Kielektroniki wa Viwango wa ZBS utatanua wigo madhubuti wa kurahisisha mchakato wa kukuza ubora wa bidhaa, kuhakikisha uwazi katika udhibiti na kurahisisha huduma kwa wazalishaji, wafanyabiashara na watumiaji kwa ujumla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Mfumo wa Viwango wa ZBS utaiwezesha Taasisi hiyo ya Viwango Zanzibar kuwa na uwezo wa kufuatilia bidhaa kwa usahihi, kuharakisha utoaji wa vyeti vya ubora na kuwawezesha wadau wote kupata taarifa kwa njia ya kidijitali jambo litakaloongeza ufanisi katika Sekta ya Viwanda na Biashara.

Aidha, Mhe. Hemed amesema Mfumo wa ISQMT umelenga kuweka Mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora na zinakidhi viwango vya Kitaifa na Kimataifa pamoja na kuondoa usumbufu ulikuwepo kwa muda mrefu hasa katika upatikanaji wa huduma kwa uwazi.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewahimiza watendaji wa ZBS kuhakikisha kuwa Mfumo wa ISQMT unatumika kwa ufanisi mkubwa pamoja na kuwataka wafanyabiashara, Wazalishaji na wadau wote wa Sekta ya Viwango kuutumia kikamilifu mfumo huo kwa lengo la kukuza ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Mhe. Hemed ametoa wito kwa wadau wote wa Sekta ya Biashara na Viwanda kushirikiana na ZBS na Taasisi nyengine za udhibiti wa viwango ili kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinakuwa na viwango bora na salama kwa matumizi ambavyo vitaiwezesha Tanzania kuwa Taifa lenye ushindani mkubwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) Ndugu Yusuph Majid Nassor amesema madhumuni ya Kuazimishwa kwa Mfumo wa Viwango Zanzibar ni kuleta ujumuishaji wa wadau wote wanaofanya kazi na ZBS ili kufanya kazi kwa ufanisi na Tija pamoja na kupunguza changamoto mbali mbali katika utowaji na upatikanaji wa huduma.

Yusuph amesema zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1.2 zimewekezwa katika uandaaji wa Mfumo huo kupitia wafadhili Trade Mark Afrika ambao utarahisisha upatikanaji wa huduma kwa njia ya kidijitali kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kanda Afrika Mashariki na Kati bibi Monica Hangi amesema Taasisi ya Trade Mark Afrika kwa Kushirikiana na Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) wameamua kuanzisha mfumo wa viwango Zanzibar kwa lengo la kuboresha mazingira ya ubora na kuweka ufanisi katika kuboresha na kuweka viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa.

Monica anesema kuzinduliwa kwa mfumo huo Zanzibar itaweza kuunganishwa na masoko ya ndani na nje ya nchi, kufanya kazi kwa uwazi, uhakika na kwa haraka jambo ambalo litachangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali.

Monica amefahamisha kuwa mfumo huo utakaokuwa na viwango ambavyo vitawasaidia wadau na wazalishaji wa bidhaa Zanzibar kuweza kutengeneza bidhaa zenye viwango vya kufikia na kukidhi matakwa ya ushindani wa Kibiashara katika Masoko ya Biashara ya ndani na nje ya nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akiwasha Kifaa maalum kwa ajili ya uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki wa Viwango wa ZBS (ISQMT) kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages