WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema serikali
inatarajia kujadili kushusha kiwango cha fedha kinachohusika katika
makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kwenye mahakama ya mafisadi ili
kukomesha vitendo vya rushwa.
Mwakyembe alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
“Nimeulizwa sana na waandishi wa habari tangu Julai hadi sasa
walitegemea kungekuwa na kesi nyingi lakini kuna kesi moja katika
Mahakama ya Mafisadi tumekuja kubaini kwamba uchache wa kesi ndiyo
mafanikio makubwa ya hatua ya kisheria tuliyochukua,”amesema.
Aliongeza kwa sasa waliozoea kupora mabilioni wamerudi nyuma ambapo
wezi hao wameonekana wakiiba fedha chini ya Sh bilioni moja iliyopo
kisheria hivyo wanategemea kujadili sheria hiyo ili iwalenge hata
wanaochukua kiasi kidogo.
“Sisi kama serikali tukiona wizi sasa umenza kupungua na kuenea
katika viwango vya Sh milioni 400, 500, 700 tumeanza kujadiliana
kuangalia uwezekano wa kushusha kiwango cha fedha ili tuweze kukomesha
kabisa udokozi, ubadhilifu, wizi wa fedha au mali ya umma,”alisema.
Aidha alifafanua uamuzi wa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda kutafuta
vijana wanaojua sheria ili kusaidia wananchi kabla ya kwenda mahakamani
ni mzuri.
Aliongeza kuwa tayari wamepeleka mswada wa msaada wa kisheria ambao
utasaidia wananchi hasa wa vijijini na wanawake ambao ndiyo wanaumizwa
na desturi zilizopitwa na muda ili kuwasaidia kupata haki na itakuwa na
wasaidizi wa kisheria nchi nzima wapatao 4,900.
Makonda alisema wamejadili utoaji na upatikanaji wa haki kwa wakati
kwani kuna changamoto ya watu kuwa wengi na kuchelewa kupata haki zao.
Alisema kwa kuona adha hiyo mkoa huo kwa kushirikiana na Wakuu wa
wilaya watajenga Mahakama za Mwanzo 20 ili kuongeza kasi za utoaji na
upatikanaji wa haki kwa wananchi endapo wanapopelekwa vituo vya polisi.
No comments:
Post a Comment