YAPO makundi mengi ya Muziki wa Bongo Fleva ambayo yaliibuka na kupotea kimyakimya lakini pia wapo wakali wa muziki huo walioibuka na kujisahau na wengine kupotea kabisa.
Miongoni mwa makundi ambayo yalikuwa tishio yaliyoibuka na kupotea ni Daz Nundaz lililokuwa likiundwa na vichwa kama Ferooz, Fundi Daz, Daz Mwalimu (Daz Baba), Lusajo, La Rhumba na Critic, Gangwe Mobb lililokuwa na Luten Kalama na Inspector Haroun.
Parklane likiwa na CP (Cpwaa), Suma Lee na mengineo. Pia katika kipindi cha mwanzoni mwa miaka ya 2000 wapo wasanii walioibuka kama Voice Wonder, D Knob, Makamua, Noorah na wengine wengi lakini kutokana na kujisahau ama kutoelekeza nguvu kubwa kwenye muziki wamejikuta wakipotea na kusahaulika.
Jambo hilo limeendelea kuwa la kawaida hadi kipindi hiki ambapo wapo wakali wa muziki huo ambao ni wazuri sana lakini kutokana na kuwa kimya kwa kipindi kirefu (kutotoa ngoma mpya) inaonekana dhahiri wameanza kusahaulika na kupotea kimyakimya kwa mashabiki wao. Makala haya yanawaanika baadhi tu ya wasanii hao ambao wanaanza kusahaulika na kupotea kimyakimya;
Ruby
RUBY
Uwezo wa kucheza na sauti ni wazi kwa shabiki yeyote wa burudani kukubaliana nami kuwa dada huyu ni tishio. Ruby alianza kujulikana rasmi Februari, 2015 alipoibuka na Ngoma ya Na Yule kisha Forever.
Hapa kati kulikuwa na misukosuko na menejimenti yake lakini Septemba mwaka jana aliibuka tena na Ngoma ya Wale Wale ambayo ilishika kiana. Tangu hapo amekuwa kimya na ngoma zake hizo tatu.
Taratibu ameanza kusahaulika na asipoangalia anaweza kupotea.
TUNDA MAN
Nani asiyemjua mshikaji huyu wa kulalamika kwenye nyimbo? Tunda alijizolea umaarufu kwenye ngoma kibao kama Neila akiwa na Chid Benz (2008), Starehe Gharama akiwa na Ali Kiba na Chegge (2011), Msambinungwa akiwa na Ali Kiba (2013). Licha ya kuwa tishio, kwa sasa ni kama amepunguza makali, ngoma yake ya mwisho ambayo ni kali ilikuwa ni Mama Kijacho iliyotoka mwishoni mwa 2015.
Tunda man
YAMOTO BAND
Moja kati ya makundi bora kabisa ya vijana kuwahi kutokea Bongo.Kundi hili linaundwa na vijana wanne, Beka, Aslay, Maromboso na Enock Bella likiwa chini ya Mkubwa Fella (Mkubwa na Wanawe). Yamoto ilianza kuchanua 2014 kuelekea 2015 wakiwa na Ngoma ya Ya Moto. Tangu hapo walikuwa wakiibuka kila baada ya miezi kadhaa na ngoma kali. Ngoma zao zilizokuwa gumzo ni Niseme na Nitajuta (2014/2015), Nisambazie Raha, Nitakupelepweta (2015) na Mama (2016). Mara ya mwisho kutoa ngoma kali ilikuwa Juni mwaka jana walipoibuka na Ngoma ya Su. Shoo zao si kama za zamani ambapo kila ‘event’ kubwa lazima wawemo.
Yamoto Band
MWASITI
Moja kati ya vichwa vya kutegemewa katika Jumba la Vipaji (THT) akisimama kama mwalimu wa wanamuziki wanaoibuka. Ngoma kama Nalivua Pendo na Serebuka alizozitoa 2014 zilimuweka kwenye ramani ya Muziki wa Bongo Fleva. Ngoma yake ya mwisho ilikuwa 'Kaa Nao' aliotoa mwishoni mwa mwaka jana ambayo haikuwa 'hit' kama nyimbo zake za nyuma.
Mwasiti
TEMBA
Temba alianza kuibuka na Ngoma ya Mpenzi Nakumind mwanzoni mwa mwaka 2000 na baada ya hapo alikuwa tishio kwa kila ngoma aliyoitoa. Miongoni mwa ngoma zilizoendelea kumpa umaarufu ni Nampenda Yeye (2005), Amekoma (2008), Kiulaini (2012) na nyingine nyingi. Mara ya mwisho kutoa hit ilikuwa miezi 10 iliyopita ambapo aliibuka na Ngoma ya Fundi akiwa amemshirikisha Jokate na Maromboso. Kusahaulika kwake kunaanza kuonekana kutokana na kuweka nguvu kubwa katika kusimamia kundi la Mkubwa na Wanawe.
Mtemba (kushoto) aliyevaa suti
ABDU KIBA
Ni mdogo wa staa wa Bongo Fleva, Ali Kiba. Kimuziki ameonesha kuwa anaweza baada ya kuibuka na ngoma matata ya Huyo Siyo Demu (2011) akiwashirikisha Nay wa Mitego na Neyba. Tangu hapo ameendelea kuliteka soko la muziki huo baada ya kuibuka tena na projekti maalum aliyomshirikisha kaka yake (Ali Kiba) ambayo ilimuibua upya na ngoma ya Kidela (2013) na Pita Mbele (2014). Licha ya kuendelea kutoa ngoma kama Ayayaa (2015) akimshirikisha Ruby ambayo haikufanya poa, mara ya mwisho kwake kutoa ngoma kali ilikuwa Juni 2016 Ngoma ya Bayoyo.
Abdu Kiba
RECHO
Alianza kutambulika 2011 na Ngoma ya Kizunguzungu akitokea Jumba la Vipaji (THT) ambapo wengi waliona mtu sahihi wa kuliziba pengo la mwanadada aliyepotea kimuziki, Ray C ni huyo. Baada ya hapo kweli aliendeleza makali yake na Ngoma ya Upepo (2012), Umependeza na Nashukuru Umerudi (2013) na Nikumbatie (2014).
Recho
Kwa kipindi kirefu amekuwa kimya kimuziki na mara ya mwisho hakuibuka na ngoma mpya bali ni kati ya watuhumiwa wa madawa ya kulevya ambapo aliwekwa selo kwa siku tatu na sasa yupo nje kwa dhamana. Ushauri wangu kwa wasanii hawa ni kwamba, babo mashabiki wanawahitaji kwa kuwa uwezo wao wa kuimba si wa kitoto, ni suala la wao kujipanga upya na kuhakikisha hawaingii kwenye orodha ya wale ambao muziki umewakataa mazima!
No comments:
Post a Comment