Mwanariadha
pekee wa Tanzania aliyeshiriki mashindano ya London Marathon yaliyofanyika muda
mfupi uliopita jijini London leo Jumapili ya Aprili 23 nchini Uingereza,
Alphonce Simbu amefanikiwa kushika nafasi ya tano (5) dhidi ya wanariadha
wenzake mashuhuri duniani.
Alphonce,
ambaye ni Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mashindano
maarufu ya Standard Chartered Mumbai Marathon, katika mbio za leo za London
ameweza kuitoa tena Tanzania kimasomaso kwani nafasi hiyo ni miongoni mwa
nafasi za ushindi katika michuano hiyo kwani ziliweza kushirikisha wanariadha
wengi zaidi wanaofikia takriban 40,000 kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.
Aidha
kwa upande wa nafasi ya kwanza imeenda kwa Mkenya, Daniel Wanjiru na
Wahethiopia wakipata nafasi ya Pili kupitia kwa Kenenisa Bekele. Kenya pia
imeweza kunyakua nafasi ya tatu kwa mwanariadha wake Dedan Karoki na nafasi ya
nne ikichukuliwa na Abel kirui.
Mwanariadha
huyo aliye chini ya udhamini wa DSTV Tanzania, awali alitamba kufanya vyema
kwani aliweza kujiandaa vya kutosha katika mbio hizo. “Nitapambana kwa nguvu
zangu zote. Ninakwenda London nikijua wazi kuwa naiwakilisha nchi yangu kwenye
mashindano haya makubwa. Nakwenda kupeperusha bendera ya Tanzania” alisema
simbu na kuongeza kuwa “Nina imani nitashinda kwani nimefanya mazoezi ya
kutosha na nina ari na moyo wa kushinda. Naomba sala za watanzania wote ili
niweze kuleta medali nyumbani” Alisema Simbu.
Pia
aliweza kuishukuru kampuni ya Multichoice Tanzania kupitia King’amuzi cha DStv
kwa kumdhamini na kuhakikisha anakaa kambini kwa muda wote huo bila shida
yoyote.
No comments:
Post a Comment