Mikoa mitatu
ya Tanga, Morogoro na
Iringa, imenufaika na kiasi cha shilingi bilioni 6.5 zilizotolewa kama mkopo na
Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) tangu benki hiyo ianzishwe mwaka 2015.
Kauli hiyo
imetolewa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali na msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti
Maalumu, Mhe. Felister Aloyce Bura, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza
kutoa huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Dodoma.
Dkt. Kijaji
ameeleza kuwa hadi kufikia mwezi Desemba, 2016, TADB imetoa mikopo ya jumla ya
shilingi 6,489,521,120 kwa ajili ya kutekeleza miradi ishirini (20) ya kilimo
katika mikoa hiyo mitatu ya Iringa, Morogoro na Tanga.
“Sambama na utoaji mikopo, Benki inatoa mafunzo kwa
wakulima ambapo hadi sasa vikundi 336 vya wakulima wadogowadogo vyenye jumla ya
wanachama 44,400 wamepatiwa mafunzo hayo katika mikoa hiyo mitatu” aliongeza
Dkt. Kijaji
Amesema kuwa
Benki hiyo inatarajia kuanza kutoa huduma hiyo kwa wakulima wadogowadogo wa
Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine jirani wenye sifa.
“Benki imepata nafasi kwa ajili ya kufungua ofisi
katika jengo la PSPF mjini Dodoma na itakabidhiwa ofisi hiyo mwezi Julai, 2017,
baada ya mkandarasi kukamilisha ujenzi wa jengo hilo” Alisisitiza
Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji
amesema kuwa tayari Benki hiyo imemwandikia barua Katibu Tawala wa mkoa wa
Dodoma ili kuomba aipatie miradi mizuri ya kilimo ambayo mkoa unapendekeza
Benki iifikirie katika zoezi la kutoa mikopo itakayoanza kutolewa mwishoni mwa
mwaka 2017.
No comments:
Post a Comment