MBUNGE wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, akiangalia
barabara kutoka Vigwaza-Mwavi iliyoharibika vibaya eneo la Buyuni hali
inayosababisha magari kushindwa kupita.
Mkazi wa Mwavi, Zainabu
Zuberi akivushwa kwenye maji yaliyokata barabara eneo la Buyuni, kwa
kubembwa shingoni.
Mbunge wa jimbo la
Chalinze Ridhiwani Kikwete, akizungumzia kero ya kuharibika kwa baadhi ya miundombinu
ya barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, ambapo mvua
iliyonyesha April 7 na 8 imesababisha kuharibu barabara ya Vigwaza-Buyuni-Mwavi
na ya Milo-Kitonga-Ruvu.
Baadhi ya wakazi wanaotumia barabara ya
Vigwaza-Buyuni-Mwavi wakipita kwa shida kutoka na barabara hiyo kuharibika
vibaya kutokana na mvua.
MVUA kubwa iliyoambata na upepo mkali,imekata mawasiliano ya
miundombinu ya barabara eneo la Buyuni, na kusababisha wakazi kutoka kata ya
Vigwaza na Mwavi jimbo la Chalinze, kupata shida.
Hali hiyo inasababisha wakazi hao, kuvushwa kwa kupata msaada wa
kubebwa mgongoni na shingoni kwa gharama ya sh.3,000 na 2,000 na pikipiki
kupitishwa kwa sh.5,000 huku magari yakishindwa kupita kabisa.
Baadhi ya wakazi hao,akiwemo Zaina Zuberi aliekuwa akienda Mwavi, alisema
wapo katika hali ngumu. “Mvua hapa bado haijanyesha,maji haya yanatokea maeneo ya Msoga
huko na kufika huku daraja la Mbiki, Buyuni na kukatiza katika hii
barabara, sipati picha mvua ikipiga hapa kwa mwezi huu”
“Barabara ni mbovu kama mnavyojionea, haipitiki, watu tunapata shida
kufuata mahitaji ya nyumbani, tatizo ni mkandarasi, barabara imejengwa bila
kuwekwa makaravati, kila akielekezwa kujenga kutokana na hali halisi ya barabara
haiwi hivyo,”
Nao baadhi ya vijana wanaosaidia kuwavusha watu na pikipiki, akiwemo
Rashid Juma, alisema tangu mvua ziharibu eneo hilo april 7 wanavusha watu kwa
maelewano kulingana na uwezo wa mtu. “Tunapata fedha kulingana na kichwa cha mtu au pikipiki, kila mtu
mmoja 3,000 au 2,000 na pikipiki 5,000” alieleza.
Aidha kutokana na mvua hizo, zimeathiri pia barabara nyingine ya
kutoka Milo-Kitonga hadi Vigwaza. Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, alitembelea
barabara hizo na kujionea hali halisi.
Ridhiwani alisema, hali iliyopo hairidhishi na kuwapa wakati mgumu
wakazi wa maeneo hayo, na ameahidi kuisimamia kero hiyo kwa kuifikisha bungeni
na halmashauri ya wilaya ya Chalinze ili lifanyiwe kazi.
Alieleza kuna kila sababu ya mkandarasi kufanya kazi kulingana na
uhalisia wa eneo husika hali inayosababisha wananchi kupata tabu na barabara
kuharibika kila wakati.
Katika hatua nyingine Ridhiwani ,aliunga mkono juhudi za ujenzi wa
darasa lililobomoka kutokana na mvua iliyonyesha april 7 ambapo amechangia
kiasi cha sh.100,000, mabati 50, mifuko ya saruji 50 na nondo 20.
Alibainisha kwamba shule hiyo imejengwa miaka 40 iliyopita hivyo
miundombinu yake pia imechakaa.
Ridhiwani alisema kuna kila sababu ya kuangalia namna ya
kukarabati shule hiyo kwani majengo yake yamejengwa miaka mingi.
Afisa mtendaji wa Kidogozero, Lilian Mbwa,alisema kila
kaya itachangia matofali mawili na kila mjumbe wa serikali ya kijiji ni tofali
10.
Hata hivyo alisema halmashauri ya kijiji itachangia jumla matofali
200 na wadau wa maendeleo matofali 300.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kaya zaidi ya 20 zimekosa makazi ya
kuishi na nyumba zaidi ya 90 ziliharibika, kubomoka na nyingine kuezuliwa
mapaa huko jimbo la Chalinze, kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali.
Maeneo yaliyokumbwa na adha hiyo ni Chalinze Mzee, Bwawa la
umwangiliaji la Msoga ambalo limetoboka, Msoga na shule ya Sekondari ya
Imperial.
No comments:
Post a Comment