Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu
Hassan ameuahidi uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na wa Mkoa wa Iringa kuwa
Serikali italifanyia kazi tatizo la ubovu wa barabara kutoka Iringa mjini Hadi
katika hifadhi hiyo ili kuongeza idadi ya watalii katika Hifadhi ya Taifa ya
Ruaha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan
ametoa kauli hiyo katika mkutano wake na Viongozi wa Hifadhi hiyo na wa mkoa wa
Iringa baada ya kufanya ziara fupi katika hifadhi hiyo pamoja na kujionea
utiririshaji hafifu wa maji katika Mto Ruaha uliosababishwa na shughuli za
kibinadamu hasa kilimo.
Makamu wa Rais amesema serikali itahakikisha barabara hiyo inajengwa
kwa awamu kwa kiwango cha lami kama hatua ya kuongeza maradufu idadi ya watalii
katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambapo kutokana na ubovu wa barabara kuelekea
hifadhi hapo idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imeendelea kupungua
kila uchao.
Kuhusu vitendo vya ujangili hifadhi hapo, Makamu wa Rais ameuagiza
uongozi wa hifadhi hiyo kushirikiana na wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo ili
kuwabaini majangili na kuwachukulia hatua ili kukomesha vitendo hivyo.
Amesema idadi kubwa ya majangili wanatoka miongoni mwa jamii
zinazozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha hivyo wananchi wakishirikishwa
kikamilifu katika kutoka taarifa za siri majangili wengi watakamatwa na
kuwajibishwa.
Awali akitoa taarifa kwa Makamu wa Rais, Kuhusu utendaji kazi wa
Hifadhi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ALLAN
KIJAZI aliiomba serikali isaidie kulinusuru bonde la Usangu ili liweze
kurejesha mtitiriko wa maji kwa ajili ya matumizi ya hifadhi hiyo na kumaliza
mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi na wananchi ambao umedumu kwa muda mrefu bila
suluhu kupatikana.
Amesema mapaka sasa TANAPA imeshatumia zaidi ya shilingi bilioni SABA
kwa ajili ya kulipa fidia wananchi na gharama nyingine ili kunusuru bonde hilo
lakini bado kuna changamoto ambazo zinaathiri usimamizi wa eneo hilo na zinahitaji
maamuzi ya serikali.
Mkurugenzi huyo Mkuu wa TANAPA pia amepongeza msukumo wa dhati wa
serikali ya awamu ya Tano katika kusimamia hifadhi ya mazingira na maliasili
kwani jitihada hizo zitasaidia kuboresha mazingira na viumbe hai kwa ajili ya
vizazi vya sasa na vijavyo.
Moja ya sehemu za Mto Ruaha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akiongea mbele ya waliohudhuria ziara hiyo
Mh.January Yusuph Makamba, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira akiteta jambo na makamu wa rahisi wakati wa ziara hiyo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akielezea jambo kwa Makamu wa rais
wakati wa ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment