Nimesoma na kuona katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu vurugu
zilizotokea tarehe 22 Aprili, 2017 katika hoteli ya Vina, Mabibo hapa Dar es
salaam, zinazosemekana kuhusisha wanachama wa CUF.
Ni ukweli usiopingika kuwa, suala la mgogoro wa uongozi katika chama
cha CUF lipo mahakamani, lakini nikiwa msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa
na kutambuliwa na jamii kuwa ni mlezi wa vyama vya siasa; nimelazimika kuwasihi
wadau wa siasa hususani wanachama wa chama cha CUF, kutambua kwamba, kuwapo kwa
shauri mahakamani siyo fursa ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, kwani
jambo hili ni uvunjifu wa sheria na linaleta sura mbaya kwa jamii.
Hivyo, ninalaani vurugu hizo, ambazo zilionekana kuvunja amani na
utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu zetu za taifa za amani na utulivu.
Pia, nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo, madhali masuala
haya yapo mahakamani hebu tuheshimu utawala wa Sheria.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hata Jeshi la Polisi lipo
kushughulikia malalamiko yoyote yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama
chochote cha siasa. Hivyo, hakuna haja ya wanachama wa chama cha CUF kukiuka
taratibu za kuendesha chama hicho au kujichukulia Sheria mkononi.
Aidha, ninaviasa vyama vya siasa kuelewa kuwa havipo juu ya Sheria,
vinapaswa kuheshimu na kufuata Sheria za nchi, ikiwamo kutunza amani na utulivu
tulionao.
No comments:
Post a Comment