WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amewaomba viongozi wa dini nchini kutumia nafasi zao kuhimiza wazazi
na walezi kuishi maisha yenye nidhamu, kuthamini kazi yenye kumpendeza Mwenyezi
Mungu na kusimamia malezi ya watoto na kuzingatia maadili ya Taifa kwa ujumla.
“Tabia na mwenendo mzuri
ni lazima uanzie katika ngazi ya familia, mtaani na hatimaye katika jamii.
Tukirudia utamaduni wetu wa zamani wa kusimamia maadili kwa pamoja, jamii yetu
itanusurika kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Waziri Mkuu ameyasema
hayo leo (Jumatatu, Aprili 24,2017) wakati akifungua kongamano kuhusu
mmomonyoko wa maadili na athari za dawa za kulevya lililoandaliwa na Baraza Kuu
la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya, lililofanyika mjini Dar es Salaam.
Amesema kila mzazi au
mlezi aone aibu, uchungu na ajutie anapoona mtoto yoyote akienda kinyume na
utaratibu wa kawaida wa maisha na ni vema wakatumia nafasi yao kwa kuwahimiza
vijana hao waishi maisha ya nidhamu na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu.
Waziri Mkuu amesema kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga jamii yenye kuzingatia
maadili nchini na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli amekuwa akiwasisitizia
Watanzania wote kuzingatia maadili katika jamii kwa kufanya kazi kwa bidii na
kujiepusha na vitendo vyote vya rushwa na ubadhirifu.
Amesema maadili katika
Taifa ni moja ya tunu muhimu kwa kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha maendeleo,
ujenzi wa umoja, amani, upendo, uvumilivu na mshikamano kwa jamii.
Amesema maadili ni nyenzo
muhimu sana katika ujenzi wa Taifa na huliepusha kuingia katika mifarakano na
migogoro. “Hivyo hatuna budi nasi kuyalinda maadili hayo kwa uwezo wetu wote,
ili tuyarithishe kwa vizazi vijavyo, kama vile sisi tulivyoyarithi kutoka kwa
waasisi wa Taifa letu,”.
“Hata hivyo, ninyi ni
mashahidi kuwa katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia vitendo vya mmomonyoko
wa maadili na matokeo yake yanaonekana dhahiri kama kuongezeka kwa vitendo vya
rushwa, kuiga tamaduni za nchi za kigeni ambazo sio njema na hazina tija kwa
jamii, na Taifa kwa ujumla”.
“Ni ukweli usiopingika
kuwa mmomonyoko wa maadili ni miongoni mwa vichocheo vinavyopelekea matumizi ya
dawa haramu za kulevya. Hivyo ni matarajio yangu kuwa mtaliangalia kwa kina
tatizo la mmomonyoko wa maadili ambalo kwa kiasi kikubwa linatuathiri kama
Taifa katika mipango ya Serikali na maendeleo ya Taifa letu,” amesema.
Hivyo Waziri Mkuu
amewapongeza viongozi wa BAKWATA kwa kuwa na wazo la kufanya kongamano hilo
lenye kulenga kujadili namna ya kurejesha maadili katika jamii. Tukumbuke kuwa
Watanzania tutaendelea kuishi kwa upendo, amani na utulivu iwapo tutazingatia
maadili.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo mstari wa mbele kuhakikisha
kuwa mapambano na vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inafanikiwa. Lengo ni
kuhakikisha kuwa waathirika wote wa matumizi ya dawa hizo wakiwemo vijana,
ambao ndio nguvu kazi ya Taifa wanakombolewa dhidi ya janga hilo.
Amesema Serikali
itahakikisha inashughulikia mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha
na dawa za kulevya bila ajizi, ambapo vyombo vyote vya kisheria vimeelekezwa
kushirikiana katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa ya kulevya kwa
kusimamia sheria ipasavyo.
Naye Kamishna Jenerali wa
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Bw. Rogers Siyanga
amewaomba viongozi wa dini kuiunga mkono mamlaka hiyo kwa sababu inafanya kazi
kubwa ambayo inahitaji msaada wa watu wote.
Kwa upande wake Mufti na
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Alhaji Abubakary Zuberi amesema viongozi wa dini
nchini wana jukumu la kukataza maovu na kuiamrisha jamii kufanya mambo mema
badala ya kuiachia Serikali pekee kufanya kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment