Mamlaka ya Hali ya Hewa
(TMA) imetoa tahadhari kwa umma kuhusu vipindi vya mvua kubwa vinavyoambatana
na upepo mkali na mawimbi makubwa katika mwambao wa ukanda wa pwani.
Katika taarifa yake ya jana saa 11:15 jioni, TMA imetoa tahadhari kuwa, kuanzia jana hadi keshokutwa
kutakuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24
vinavyoambatana na upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa
yanayozidi mita mbili.
Mamlaka hiyo imesema
maeneo yanayotarajiwa kuathirika ni mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi
na Mtwara. Pia, visiwa vya Unguja na Pemba.
“Hali hii inatokana na
kuimarika kwa ukanda wa mvua nchini na kuimarika kwa mgandamizo mkubwa wa hewa
katika Bahari ya Hindi eneo la kisiwa cha Madagascar, hivyo kusababisha upepo
mkali katika pwani ya Tanzania,” imesema taarifa hiyo.
TMA imewataka wakazi wa
maeneo hayo kuchukua tahadhari na hatua stahiki na kwamba, inaendelea
kufuatilia hali hiyo na itatoa mrejesho kila itakapobidi.
No comments:
Post a Comment