Takribani
shilingi milioni 271 zinadaiwa kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma Mjini, Mkoani
Mara ikiwa ni kodi ya Pango la Ardhi.
Hayo
yamebainishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
alipofanya ukaguzi wa mfumo wa kodi ya ardhi hivi karibuni Mkoani humo.
Waziri Lukuvi
alisema kuwa amekagua mfumo wa kodi wa manispaa ya Musoma mjini ili kuhakikisha
wamiliki wote wa ardhi nchini wanalipa kodi kwa hiari kabla ya hatua za
kisheria hazijafuata dhidi yao.
“Nimeagiza kesi za madai ya kodi zitolewe hukumu
ndani ya siku moja tu ili wadaiwa waweze kuchukuliwa hatua ya kuuzwa kwa mali
zao haraka”, alisema Lukuvi.
Aidha Waziri
Lukuvi alimtaka Afisa Ardhi wa Manispaa ya Musoma Bw.Joseph Kamonga kuwasilisha
majina ya wadaiwa hao katika Mahakama ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria
ikiwa ni pamoja na kupiga mnada majengo na mali zao kama wakikaidi kulipa kodi
hiyo.
Kwa upande
mwingine Lukuvi alifanya uzinduzi wa mpango kabambe (Master Plan) wa Manispaa
ya Musoma na kuwapongeza viongozi na watendaji wa Manispaa hiyo kwa kuwa
Manispaa ya kwanza nchini kuweza kuzindua mpango huo kutumia kampuni za ndani
katika utekelezaji wa mpango huo.
Kufuatia
hatua hiyo Waziri Lukuvi amezitaka Manispaa nyingine kutumia kampuni za ndani
ya nchi ambazo zimesajiliwa na Wizara ya Ardhi katika kutekeleza mipango
mbalimbali ya ulipaji kodi za ardhi.
Pia Waziri
Lukuvi aliiagiza Manispaa ya Musoma kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa
mpango kabambe kwa kutumia wataalam wao (wa serikali) au Makampuni ya ndani na
kutoa nakala za kutosha ili mpango huo uwafikie wadau wote na kutaka mpango huo
utafsiriwe kwa Kiswahili ili Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa waweze
kuwafikishia wananchi kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment