Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga
akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Yun Byung-se.
Mhe. Mahiga alikuwa nchini humo kwa ziara ya kikazi ikiwa pia ni sehemu ya
maadhimisho ya miaka 25 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na
Jamhuri ya Korea.
Mhe. Balozi Dkt.
Augustine Philip Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki alifanya ziara ya
kikazi jijini Seoul, Jamhuri ya Korea tarehe 24 Aprili 2017 kwa mwaliko kutoka
kwa Mhe. Yun Byung-se, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea. Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni
sehemu ya maadhimisho ya
miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na
Jamhuri ya Korea mwaka 1992.
Wakati wa ziara
hiyo, Mheshimiwa Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake
Mhe. Yun Byung-se
ambapo Waziri Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya
Korea kwa kumpatia mwaliko wa kutembelea taifa hilo hususan wakati huu
inapoadhimishwa jubilee ya miaka 25. Mhe. Mahiga aliishukuru Serikali ya
Jamhuri ya Korea kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kimkakati katika uwekezaji
kwa kipindi cha kuanzia 2016 -2020.
Kwa kipindi cha miaka 25, Serikali ya
Korea imeisaidia Tanzania kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Ujenzi
wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi unaojumuisha
madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa meta 275 pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa
48; Ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 600 imejengwa na
kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya digitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya
Tehama zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalum kwa ajili ya
kupimia magonjwa ya wanawake.
Vilevile, Ujenzi wa Hospitali ya mama na mtoto
Chanika yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 160
inatarajiwa kufunguliwa siku za karibuni.Aidha, Watanzania zaidi ya 1000
wamenufaika kwa kupata ufadhili wa kusoma katika vyuo mbalimbali vya Jamhuri ya
Korea.
Waziri Mahiga pia alikutana na baadhi ya Wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara
wa Jamhuri ya Korea ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza
fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania mathalani ujenzi wa Reli ya Kati katika
viwango vya kimataifa; uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme; ujenzi wa
maeneo ya viwanda; na huduma ya kutoa ushauri katika miradi mikubwa.
Aidha, Mhe. Waziri aliwahakikishia
wawakilishi wa makampuni ya Jamhuri ya Korea kuwa, Tanzania imeboresha
mazingira ya uwekezaji na biashara pamoja na taasisi muhimu zinazotoa huduma
mbalimbali katika sekta hiyo.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mahiga
alitumia fursa hiyo kukutana na Balozi Sul Kyung-hoon Makamu wa Rais wa KOICA ambapo
aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuipatia zaidi misaada Tanzania kwa uwazi na bila
ya masharti yeyote. Pia aliipongeza KOICA kwa kushirikisha jamii kuanzia wakati
wa ubunifu wa mradi hadi kufikia utekelezaji pamoja na usimamizi.
KOICA wameombwa kuongeza maeneo ya
misaada na kujumuisha maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya maji na nishati ya
umeme wa jua, upepo na maji kwa ajili ya kusaidia maeneo ya vijijini. Aidha,
Mhe. Waziri Mahiga alishauri KOICA kuangalia uwezekeno wa kuanzisha vituo vya
kilimo cha kisasa, vituo vya kufugia na vituo vya kufundisha ujasiriamali ili
jamii kubwa ya Watanzania iweze kunufaika.
Katika jitihada za kutafuta washirika
kwa ajili ya kusaidia kuboresha Chuo cha Diplomasia, Mhe. Waziri akiwa Seoul
alitembelea Chuo cha Taifa cha Diplomasia cha Jamhuri ya Korea na kufanya
mazungumzo na Balozi Paik Ji-ah, Kaimu Mkuu
wa Chuo. Lengo kuu lilikuwa kujifunza uendeshaji wa Chuo, mitaala iliyoandaliwa
kutoa masomo, walengwa wa masomo hayo, aina ya wakufunzi, lugha zinazotumika
kufundishia, utaratibu wa kuandaa wanadiplomasia na mifumo ya chuo hicho.
Vilevile kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mhe.
Waziri alikutana na Jumuiya ya Watanzania waishio Jamhuri ya Korea ambapo
aliwahimiza kuheshimu Sheria na Taratibu za nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuleta
utaalam utakaosaidia kuiendeleza Tanzania.
Aidha, akizungumza na Watanzania hao ambao
wengi wao ni wanafunzi, Mhe. Waziri aliwasihi kuzingatia masomo ili kufikia
malengo waliyojiwekea na kuleta faida kwa familia zao na taifa kwa ujumla.
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliwahakikishia Wanajumuiya hao kuwa
Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufungua Ubalozi wa Tanzania jijini
Seoul na kuwaomba kutoa ushirikiano kwa Balozi wa kwanza wa Tanzania katika
nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment