UNABII HAUTAFSIRIWI KAMA APENDAVYO NABII - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Thursday, May 25, 2017

UNABII HAUTAFSIRIWI KAMA APENDAVYO NABII

Hivi sasa kuna wimbi la manabii wengi ambao wanawatabiria watu mambo yao binafsi kama wapendavyo manabii husika. Mtindo unaotumika ni baadhi ya manabii hao kujitangaza kuwa wana uwezo wa kuwatabiria watu mambo yao binafsi kwa wakati walioupanga wao na kwa tozo au malipo waliyojipangia wenyewe.
“Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” (2 Pet.1:20-21)
Hapa mtume mkuu Petro aliandika kuhusu mchakato uliotumika wa kuleta unabii kutoka kwa Mungu akisema kwa msisitizo ya kwamba “unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu”!
Katika toleo la Biblia la Kiingereza cha Amplified limeandika: “..no prophecy of Scripture is a matter of or comes from one’s own personal or special interpretation, for no prophecy was ever made by an act of human will….”
Mkazo wa Petro ulikuwa unatahadhari kuhusu tabia ya watu binafsi waliokuwa wakiibuka na kujitangaza kuwa ni manabii lakini nabii zao zinatabiri kinyume na unabii wa kimaandiko uliyokwisha kutabiriwa na manabii waliotangulia.
Wimbi la manabii wa kizazi hiki linatoa unabii kwa watu binafsi kwa ajili ya mambo ambayo ni maslahi binafsi ya kimwili; wakati unabii wa kibiblia katika Agano Jipya ulitolewa kwa ajili ya kuwajenga waamini katika mambo ya rohoni na kuimarisha imani zao kwa Mungu.
Mashaka makubwa yanayoliandama wimbi la manabii wa kizazi hiki, ni kukwepa kurejea na kujipima kihuduma na nabii za kibiblia zilizoanidkwa katika Agano Jipya zikitabiri matukio ya hukumu za Mungu kwa wakati wa mwisho! Manabii wa kizazi wamejikita katika kuwatabiria watu mambo mema tu na ahadi za mafanikio ya kidunia kana kwamba imani ni kwa ajili ya mafanikio ya kimwili peke yake!
ONYO KALI KUHUSU TAFSIRI POTOFU YA UNABII
Jambo la kutisha lakini halionewi hata aibu,na linashabikiwa na wengi ni hizi tozo wanazotoza manabii kwa wale wanaowatabiria mambo yao. Sasa umefika wakati wa kurejea kwenye nabii za kibiblia, ili kupata tafsiri sahihi na makini, ili kuwaonya watu wajilinde na kujiepusha na makatazo ya kweli ya kinabii.
“Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, mtu yeyote akiyaongeza, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.” (Ufu.22:18-19)

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages