Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesimamisha umiliki wa mwekezaji wa
mashamba ya katani yanayomilikiwa na kampuni ya Le-Mash Enterprises Limited
yaliyopo kata ya Mnazi wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Waziri Lukuvi amefikia
uamuzi huo baada ya wakazi wa eneo hilo kuzuia msafara wake na kupata
malalamiko mengi kutoka kwa wananchi hao na viongozi wa Halmashauri ya wilaya
ya Lushoto wakimlalamikia Waziri kuhusu mashamba matatu ya Mnazi
yaliyotelekezwa na mmiliki wa mashamba hayo bila kuendelezwa na kusababisha
migogoro kwa awakazi wa Mnazi.
Baada ya kupokea
malalamiko hao Waziri Lukuvi aliamua kutembelea mashamba hayo na kuyakagua ili
kujionea hali halisi na kuwasikiliza wananchi ambao wamekuwa wanakabiliwa na mgogoro
huu kwa miaka mingi.
Baada ya kutembelea na
kujiridhisha Waziri Lukuvi amesema kwamba shamba hilo linastahili kufutwa kama
ilivyopendekezwa na ofisi ya Mkoa wa Tanga na ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda
ya Kaskazini kwa kuwa mmiliki ameshindwa kuwa na sifa za umiliki kwa kuwa
hajalipa kodi ya ardhi tangu mwaka 2004, hajalipa wafanyakazi wake kwa muda
mrefu, miundombinu yake na mazingira ya kazi hayaridhishi na ameshindwa
kuliendeleza shamba hilo tangu akabidhiwe mwaka 1997 kwa kurithi mashine na mitambo
ileile ya mkoloni ya mwaka 1937.
Aidha, katika ziara hii
Waziri Lukuvi amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela na Mkuu wa
Mkoa wa Manyara Mhe. Joel Bendera ili kutatua migogoro ya mipaka iliopo kati ya
Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara na Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga ikiwa ni
muendelezo wa mikutano ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro huu ambao umesababisha
uvunjifu wa amani.
Waziri Lukuvi anatekeleza
agizo la Waziri Mkuu Mhe. Khassim Majaliwa ambae alimuagiza Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kutatua mgogoro huu uliodumu
kwa miaka mingi kati ya Wilaya hizo mbili pindi alipofanya ziara yake mkoani
Tanga.
Mnamo tarehe 18 Januari,
2017 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara Wilayani Kilindi katika
Kijiji cha Mafisa na kuzungumza na wanachi Kijijini hapo kuhusiana na mgogoro
huo na kutoa maagizo kwa viongozi wa kuchaguliwa kuacha kutumia nafasi zao
vibaya kuongoza kwa mihemko au ushabiki kwa kuwa kufanya hivyo kunapelekea
wananchi kufuata ushabiki na kuvunja sheria zilizopo.
Ili kutekeleza agizo hili
wakuu wa mikoa hii miwili wakiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi wamekutana ikiwa ni muendelezo wa vikao vya
kulitafutia ufumbuzi suala hili.
No comments:
Post a Comment