Mhubiri
mashuhuri wa Neno la Mungu Tanzania, Nabii Nicolaus Suguye, ameliamsha “dude”
kwa kutangaza oparesheni maalumu ya kusambaratisha majini na nguvu za giza
Tanzania, itakayoanzia jijini Dar es Salaam na kuenea nchi nzima.
Nabii
Suguye ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya The Word of Reconciliation
Ministries (WRM) mara kwa mara amekuwa akifanya utumishi wake jijini Dar es
Salaam, ambapo katika ibada zake, matendo makuu, ishara na maajabu vimekuwa
vikishuhudiwa.
Akitangaza
oparesheni hiyo Dar es Salaam hivi karibuni, Nabii Suguye alisema kuwa Mungu
amemtuma kuwafungua watu wake waliofungwa katika magereza ya nguvu za giza nchi
nzima na oparesheni hiyo kubwa, itazinduliwa tarehe 27 ya Mwezi Septemba, 2017
katika Viwanja vya Hali ya Hewa, Ukonga Banana, jijini Dar es Salaam, kasha kuendelea
katika mikoa mbalimbali Tanzania.
“Nilikuwa
kwenye maombi, Mungu alinionyesha watu wake wakiteseka katika mateso makali ya nguvu
za giza. Kisha nikasikia sauti ikiniambia kuwa nimetumwa mimi kwenda
kuwakomboa, ndio maana kanisa letu limeamua kutekeleza oparesheni hii kwa
kuanzia na siku tano za mapambano zitakazoshuhudia ushindi mkuu kwa waaminio”,
alisema Nabii Suguye.
Alisema
kuwa, pamoja na kuzindua oparesheni hiyo ya kukabiliana na majini na wale
wanaoyafuga, pia watatumia mkutano huo kumshukuru Mungu kwa ajili ya amani
ambayo ameipa Tanzania kama zawadi ya pekee.
Akifafanua
Nabii Suguye alisema kuwa amani ya Tanzania ni matokeo ya neema ya pekee kutoka
kwa Mungu na ataongoza maelfu ya Watanzania kupaza sauti zao juu kumpa Mungu
sifa na utukufu kwa kuilinda nchi na kuiepusha na mabalaa.
Kanisa
la WRM ni miongoni mwa makanisa yanayokuwa kwa kasi ya ajabu, huku likiendesha
huduma maalumu ya maombi na maombezi kwa watu kutoka ndani na nje ya Mkoa wa
Dar es Salaam na nje ya nchi pia; likiwa na hosteli maalumu za kuwapokea
wagonjwa na wenye kuteswa na ibilisi.
Shuhuda
za matendo makuu ya Mungu yanayotendeka kupitia mikono ya Nabii Suguye,
zimekuwa zikionekana kupitia kituo cha luninga cha huduma hiyo kiitwacho WRM
TV, ambayo inapatikana kwenye king’amuzi cha Azam, Startimes na Satelite na
kuwa mchango mkubwa katika ujenzi wa ufalme wa Mungu.
No comments:
Post a Comment