Benki ya NMB kupitia sera yake ya Uwajibikaji kwa Jamii kwa kushirikiana na British Council na WGI Tanzania imekabidhi kompyuta 10 pamoja na maktaba ya kidigitali kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kisutu iliyopo Ilala Jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Kitengo cha Uwabikaji kwa Jamii (CSR) cha benki ya NMB, Lilian Kisamba amesema msaada huo umelenga kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza na kuimarisha somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchi nzima.
“Kwa miaka mingi sasa NMB tumekuwa wadau wakubwa katika kusaidia matatizo mbalimbali yanayoikabiri jamii. Tumejikita hasa katika maeneo ya elimu, afya na utoaji wa elimu juu ya masuala ya kifedha. Msaada huu wa kompyuta unalenga kuunga mkono juhudi za serikali katika kufikia malengo ya kuinua somo la tehama(ICT),” amesema Kisamba na kuongeza.
“Hii ni sehemu ya muendelezo wa utekelezaji wa sera yetu ya kusaidia jamii, kwa miaka mingi tumekuwa tukifanya hivyo mfano mwaka jana tulitoa kompyuta 300 ambazo 250 zilisambazwa Tanzania Bara na 50 zikasambazwa Zanzibar. Kwa mwaka huu pia tumetenga kompyuta 300 ambazo tutazitoa kwa shule za msingi na sekondari nchi nzima.”
No comments:
Post a Comment