Morani mmoja katika kaunti ya Kajiado nchini
Kenya ameacha watu midomo wazi baada ya kufunga ndoa na wanawake wawili kwa
mpigo.
Tom Makui, maarufu kama Junior, 27, alifanya sherehe hiyo ya
harusi Jumanne wiki hii.
Ameambia Mwandishi wa BBC Anne Ngugi kwamba sasa watu wameanza
kumbandika majina ya ajabu.
"Nimeitwa Simba na hata Dume," amesema.
Makui anatokea kwenye familia ambayo ndoa za wake wengi ama
mitala ni jambo la kawaida.
Hata hivyo kuoa wake wawili kwa mpigo ni jambo
ambalo halikuwahi kusikika katika jamii ya Kimaasai ambayo wanandoa hao
wametokea. Wapo wanaume wanaowaoa wake wengi lakini si kwa wakati mmoja.
Katika harusi hiyo ambayo ilipambwa vilivyo katika kitongoji cha
Kisaju, Mako aliwaoa Elizabeth Silamoi, 25, na Joyce Tikoyo, 23.
Wote wawili ni wanafunzi wa chuo kikuu cha Kenya Assemblies of
God mjini Kitengela, si mbali sana na eneo Kisaju anakoishi Tom.
Huhudhuria masomo na kurejea nyumbani jioni. Wamekuwa pamoja kwa
mwaka mmoja, na sherehe ya Jumanne ilikuwa ya kurasmisha ndoa kati ya
kitamaduni.
Ana wasiwasi kuhusu kutosheleza mahitaji ya wawili hao?
"Nina uhakika kuwa nitaweza kuwatosheleza wake wangu
wawili, najua wana umri ambao kila mwanamke anahitaji mume wake, lakini mimi
sijichanganyishi na vileo wala sigara au madawa ya kulevya kwa hivyo nitaweza
kazi zote kuwaridhisha wake wangu," anasema Makui.
"Mambo ya kule ninakoishi sana sana mimi ninaamua jioni
nitakapolala, hakuna siku nimegawanya wala nini, mimi hupiga simu na kumueleza
mke mmoja kuwa siji kwake na ninakwenda kwa mwenzake wako majirani ndani ya
boma langu."
Mako alikutana na Bi Silamoi miaka miwili
iliyopita wakati akichunga ng'ombe wake karibu na nyumabni kwa mwanamke huyo.
Mwaka jana akakutana na Bi Tikoyo pia akiwa
anachunga ng'ombe karibu na kwao.
Katika mila za Kimasai, mahari ya ng'ombe hutolewa kabla ya
kufungwa kwa ndoa, na bwana harusi Makui alikamilisha hilo ipasavyo.
Mako aliwaoa wakeze kimila japo wote walivalia mavazi ya
kimagharibi. Makui alivalia suti ya rangi ya samawati na wakeze wakivaa mashela
meupe. Wote pia walivalia urembo wa Kimaasai.
"Nataka kuliweka sawa hili, harusi yangu
ilikuwa ya kimila na haikuwa na mahusiano yoyote na kanisa. Kuna watu wanatuma
habari za kupotosha mitandaoni kuwa ndoa yangu ilisimamiwa na wachungaji,"
Makui, ambaye ni mfanyabiashara, awali aliambia gazeti la kibinafsi la Star la
nchini Kenya.
Amesema amewaoa wanawake
hao kwa sababu wote wanampenda na hakutaka kumsononesha yeyote kati yao.
"Huu ni ujumbe ninaoutuma kwa waume wa kisasa wanaojifanya
kuwa wanampenda mwanamke mmoja na huku wakiwalaghai kwa kuingia kwenye
mahusiano na wengine pembeni," amesema.
"Nimekuwa muaminifu kwa wake zangu kwa sababu sitakuwa na
sababu ya kuongeza mke mwengine. Ninaamini wawili watanitosheleza."
Wake hao wawili
wanapendana?
Bi Silamoi ndiye aliyekuwa wa kwanza kuingia kwenye penzi na
Makui, na kusema kabla ya kuja kwa mwenzake wawili hao walijadiliana kwa kina
na kukubaliana.
"Ninampenda. Nilimpa
Baraka zangu kuongeza mpenzi. Nampenda (mke mwenzake) pia."
Mke wa pili Bi Tikoyo
alipoulizwa na BBC kuhusu kuingia kwake kwenye uhusiano huo, alisema:
"Hapa mimi sijakuja
kuharibu ndoa , tulisikilizana wote na mke mwenza hakuwa na matatizo yeyote na
mimi, mimi nilipenda mumewe wangu tu nilipomuona na sina wasiwasi wakuwa tuko
wawili "
Naye Mke wa Kwanza
alipoulizwa ikiwa hana wivu kuwa ana mwenza, alisema:
"Ndio wivu lazima
uwepo kwa kuwa sisi ni binadamu lakini kwa kuwa ninampenda mume wangu
nimekubali tu, ndio ndoa ina changamoto nyingi lakini kwa yote ninamtumainia
Mungu."
Bi Tikoyo, amesama wote
wamekubaliana kuwa katika mahusiano ya aina hiyo na wazazi wake walikubali hilo
kwa sababu wanamuamini Makui.
Wazazi wa bwana harusi, Bw Makui Busabus na Bi
Sintiyio, wamesema hawakuamini mwanzoni mtoto wao alipowaambia anataka kuoa
wake wawili kwa siku moja, na sherehe moja. Lakini hilo limepita.
"Kwa umri wangu wa
miaka 90 sijawahi kuona kitu kama hiki huku umasaini. Kwa kawaida, mtu
anayetaka kuongeza mke husubiri kwanza walau baada ya mwaka au miaka miwili
toka alipofunga ndoa ya kwanza," amesema Busabus.
Mamorani wengine pamoja na wageni waliohudhuria harusi hiyo
wanamchukulia Makui kama shujaa kwa kufanya jambo ambalo halikuwahi kufanyika
kabla Umasaini.
Baadhi wanasema ameonyesha ukomavu, na hata anafaa kugombea
wadhifa wa diwani na baadaye hata awe gavana wa jimbo.
Baada ya harusi, watatu hao wamekuwa
wakiendelea na maisha yao.
Ingawa Bi Silamoi na Bi Tikoyo wanatokea ukoo
mmoja, hawajatokea familia moja.
No comments:
Post a Comment