Benki ya Exim mwishoni mwa wiki iliandaa chakula maalum kwa ajili ya wateja wake jijini Tanga ili kutoa wasaa wa kujadili fursa za kibiashara, mipango ya ukuaji na huduma zitolewazo na benki hiyo katika jiji hilo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyohudhuliwa na wadau mbalimbali wa benki hiyo wakiwemo viongozi wa kiserikali, wafanyabiashara wakubwa na wadogo pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo, Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Exim Bw Jaffari Matundu alisema kupitia hafla hiyo walilenga pia kutoa fursa miongoni mwa wateja hao ili waweze kufahamiana na kufungua wigo wa kufanya biashara pamoja.
“Pamoja na kushukuru kwa namna ambayo wateja wetu wamekuwa nasi hadi kufikia mafanikio ya kuikuaji na ubora wa huduma zetu, hafla hii inatoa fursa kwa wateja wetu pia kufahamiana wao kwa wao na hivyo kufungua milango ya fursa baina yao,’’ alisema Matundu.
Alisema ukuaji wa benki hiyo unaoshuhudiwa kwasasa ni matokeo ya ushirikiano baina yake na wateja wake ambao kwa kiasi kikubwa wameonyesha imani kubwa kwa benki hiyo hali ambayo imekuwa ikiiwezesha benki hiyo kubuni huduma bora na rafiki za kibenki ili kulinda na kurejesha imani hiyo kwa wateja wa benki hiyo.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997 benki hiyo imezidi kujitanua ndani na nje ya nchi ambapo hivi karibuni ilionesha nia na utayari wa kuinunua rasmi benki ya UBL Tanzania Limited (UBTL) kwa asilimia 100 baada ya kusainishana barua ya kuonesha nia (Letter of Intent).
“Kwa muda wote wa uwepo wake ndani na nje ya nchi benki ya Exim imekuwa ikijipambanua kwa ubora wa huduma ikilenga kujenga thamani ya uwekezaji kwa wadau wake na kufikia ukuaji wake kwa kutoa huduma kwa upekee na iliyoboreshwa. Haya yote yamekuwa yakifanikiwa kwa urahisi sababu utekelezaji wake umekuwa ni jumuishi kwa kuwa unahusisha wadau wote kwa majadiliano na wateja wetu kama hivi,’’ alisema.
Pamoja na mambo mengine hafla hiyo ilipambwa na shuhuda mbalimbali kuhusu ubora wa huduma za benki hiyo kutoka kwa wateja mbalimbali wa benki hiyo.
Meneja Uendeshaji wa Benki ya Exim Bi Doreen Mcharo (katikati) akizungumza na baadhi ya wateja wa benki hiyo wakati wa tafrija ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki yaExim kwa ajili ya wateja wake wa jiji la Tanga iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini humo.
Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Exim Bw Jaffari Matundu akizungumza na baadhi ya wateja wa benki hiyo (hawapo pichani) wakati wa tafrija ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki yaExim kwa ajili ya wateja wake wa jiji la Tanga iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini humo.
Mmoja wa wateja wa benki ya Exim Tanzania jijini Tanga Bi Anna Saimo akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mmoja wa wateja wa benki ya Exim Tanzania jijini Tanga Bw Sifaeli Mafunga akizungumza kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa banki ya Exim tawi la Tanga pamoja na Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Exim Bw Jaffari Matundu, kwenye picha ya pamoja mara baada ya hafla hiyo.
No comments:
Post a Comment