
Daktari Bingwa Upasuaji (plastic surgery), Dkt. Ibrahim Mkoma wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu huduma ya matibabu ambayo Bi. Mariam Rajab Juma ameanza kupatiwa katika hospitali hiyo.
Wataalam wabobezi wa Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH), leo wameanza kufanya vipimo mbalimbali vya uchunguzi kwa
Mariam Rajab Juma mwenye kidonda sehemu ya mgongoni ili kubaini chanzo cha
ugonjwa alionao.
Akizungumza na Wanahabari juu ya
mwenendo wa matibabu ya Mariam, Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Ibrahim Mkoma
amesema vipimo hivyo ni pamoja na kuchukuliwa sampuli ya nyama kutoka sehemu ya
kidonda na kupelekwa maabara kwa watalaam wa patholojia ili kubaini kama kuna
saratani au la.
Aidha Mariam ameandikiwa kufanya
vipimo mbalimbali ikiwemo CT-scan ya kifua na kichwa, Ultrasound pamoja na
vipimo mbalimbali vya damu.
Dkt. Mkoma amesema kidonda kilichopo
sehemu ya mgongo wa Mariam ni kidonda sugu na kwamba hadi sasa haijabainika
kama mgonjwa huyo ana tatizo la saratani au la mpaka hapo majibu ya
wapatholojia yatakapo patikana ndani ya siku nne kuanzia sasa.
Mariam amesema aliwahi kuugua moto akiwa
na umri wa miaka mitano ambapo alitibiwa na kupona ingawa alibaki na kovu kubwa
kuanzia sehemu ya mgongo wake hadi kwenye kisogo.
Amesema mwezi wa nane mwaka jana
alipata kipele kwenye kovu na baadae kipele hicho kugeuka kuwa jipu.
Alipotumbua jipu lilitoa usaha na kisha kuanza kuota kidonda kilichoendelea
kuongezeka siku hadi siku.
“Nilienda kutibiwa katika Hospitali ya
Makiungu iliyopo Manispaa ya Singida, lakini pia kutokana na wazazi wangu
kutokua na uwezo wa kifedha niliacha kwenda hospitalini na kuanza kusafisha
kidonda mwenyewe, huku nikiwaomba marafiki zangu niliosoma nao sekondari
wanichangie fedha ili niweze kununua dawa,” amesema Mariam.
Amesema wakati anatibiwa katika
Hospitali ya Makiungu wataalam walimshauri kuja Muhimbili ili kupatiwa matibabu
zaidi, lakini kutokana na wazazi wake kukosa fedha alimtafuta rafiki yake
aitwaye Seif ambaye pia alisoma naye sekondari akamrekodi kwa simu yake na
kutuma kwenye mitandao ya kijamii na huo ukawa mwanzo wa yeye kuanza kupata
msaada.
Mariam anaishukuru Serikali kupitia
kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
na Menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuitikia wito wa kumsaidia
na kuanza kumpa huduma.
Aidha, anawashukuru Watanzania kwa
jinsi walivyompigia simu na kutaka kumsaidia baada ya kuona picha ya video
kwenye mitandao ya kijamii.
No comments:
Post a Comment