Na Paul R.K Mashauri
Kwa tathmini yangu ya haraka, kwa sasa
takribani 80% ya rafiki zangu katika "corporate world" wanafanyia
kazi nyumbani. Miaka michache iliyopita hata kabla ya COVID-19 takwimu za New
York Times zilikuwa zinaonyesha kwamba idadi ya watu wanaofanya kazi zao nje ya
ofisi (nyumbani, katika migahawa nk) kwa lugha ya kitaalam "remote
workers" ilikuwa ni 3% tu. Lakini idadi hiyo ilikuwa imekuwa kwa ongezeko
la 80%. Sina takwimu za sasa baada ya janga la COVID-19 lakini inawezekana
idadi ikawa imeongezeka zaidi.
Pamoja na kwamba tuko katika kipindi kigumu, bado
kuna jema la kujifunza. Wiki chache zilizopita nilikutana na dada mmoja ambaye
nilisoma naye somo la "Political Science and Public Administration"
pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-Mlimani. Nikamuuliza unafanya kazi wapi?
Akasema sifanyi kazi. Nikamuuliza kwanini? Akasema kwa sababu mtoto wangu mmoja
"anaumwa" na anahitaji uwepo wangu muda mwingi nyumbani.
Nilisikitika kwa ajili ya mtoto lakini pia kwa
ajili ya "potential" ambayo ilikuwa inapotea. Yule binti namjua
vizuri na ana kichwa kizuri, mchapa kazi na mbunifu "very creative".
Wapo wengi ambao walikuwa wanatamani kufanyakazi lakini kutokana na changamoto
fulani fulani hawawezi kufanya kazi ofisini. Imewabidi kukaa tu nyumbani. Dunia
imejifunza kuwa kumbe inawezekana watu wakafanyia kazi nyumbani. Katikati ya
janga tumefunguliwa macho. Kumbe hata rafiki yangu mwenye mtoto mgonjwa
nyumbani na wengine wa namna yake bado wanaweza kuajiriwa na kufanya kazi
nyumbani "remote workforce"
Lakini zaidi ya wenzangu ambao walishindwa
kuajirika kwa sababu hawawezi kutoka nyumbani, kuna kazi ambazo hazihitaji mtu
kwenda ofisini; mfano "data entry", IT "professionals",
"rasilimali watu", "waandishi wa miradi" "copy writers"
nk. Hata janga la COVID-19 litakapoisha yamkini makampuni mengi yakachukua
hatua za kuendelea na utaratibu wa watu kufanyia kazi majumbani. Kwanini?
1. Kwanza inapunguza gharama za kuwaweka watu
ofisini. Kumbuka kila mfanyakazi anapokuwa ofisini lazima AC zote ziwashwe,
maji ya kunywa nk.
2. Inapunguza gharama za usafiri kwa wafanyakazi.
Kumbuka makampuni mengi yanawalipia wafanyakazi wao gharama za kuja na kuondoka
ofisini
3. Inaondoa nafasi ya watu kupika majungu
"office politics". Kumbuka watu wanatabia tofauti na wanatoka katika
tamaduni tofauti. Kwa mantiki hiyo watu wenye "sumu kali" sana
wanapokuwa ofisini kazi yao ni kusengenya wengine na kutafuta namna ya
kumuondoa huyu na yule ilimradi tu wanafanya "siasa". Ukiwa nyumbani
utafanya "siasa" na nani?
4. Kuna watu wanatumia ofisi "kuchepuka"-he
he he he!. Ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu ya wanandoa kuwa na mahusiano ya
"kigaidi" maofisini kwao hasa kati ya mabosi na wasaidizi wao, ma
"sugar dady" na mabinti waliotoka chuo wenye tamaa za "promotions
na magari" bila kusahau ma "sugar mammies" na viserengeti boys
"marios" vijana ambao wametoka vyuoni wanataka maisha ya
ghaflaghafla"
Kwa udadisi wangu kutokana na taaluma yangu ya
"sociology" ugaidi mwingi unafanyika wakati wa "lunch time"
au muda wa ziada baada ya muda wa kazi. Kuna watu wanabaki ofisini wakijidai
wanapenda sana ofisi kumbe wanafanya ugaidi. Kwahiyo kufanyia kazi nyumbani
inasaidia sana kuimarisha ndoa na kuondoa "nuksi" maofisini.
Hata "marufuku" ya kusafiri itaokoa sana
ndoa. Angalau kwa kujitafakari. Kweli "mtu unatoka Dar es Salaam, m
"mama" au m"baba" unasema wewe ni "mjasiriamali"
unapanda ndege kwenda China familia yako inafurahi imepata mpambanaji kumbe
humo kwenye ndege "umemlipia" na mchepuko wako ili mkutane China"
Kweli?
Tena kwenye ndege mnajifanya hamfahamiani wewe
unaongea kimakonde yeye anaongea kipare! kweli? wakati China mnaenda hoteli
moja! Kweli? Ndio maana nasema, katikati ya janga hili la COVID-19 kuna mengi
ya kujifunza. Ni kweli uchumi unayumba lakini katika eneo la ndoa jamani tuseme
ukweli kuna faida na mengi ya kujifunza!
Lakini pamoja na faida hizo pia kuna changamoto
zake hasa makazini. Kufanya kazi na watu wakiwa nyumbani kunahitaji uwekezaji
katika teknolojia mfano "collaboration tools". Nilikuwa naangalia
gharama ya "Group Wise Email" nikakuta ni hela nyingi sana. Kwa hiyo
hizi teknolojia pia zinahitaji fedha.
Ina maana lazima kampuni ifanye "cost-benefit
analysis" kufanya maamuzi ya teknolojia gani itumike. Zaidi ya hapo
unahitaji kuchagua sana wafanyakazi kabla hujawapa ajira. Hivyo lazima upate
watu ambao hawahitaji usimamizi wala kusukumwa kufanya kazi
"self-motivated employees". Lazima wawe wenye kuipenda kazi yao sio
kupenda kukaa ofisini kupiga sogo.
Kingine ni changamoto ya muda. Kumbuka ukitaka watu
wafanye kazi wakiwa nyumbani wakati mwingine utakuta watu wanaishi maeneo
tofauti. Kwa mantiki hiyo wakati John kwake ni mchana, Amina kwake ni usiku.
Hapa nimefikiria makampuni ambayo yana "wafanyakazi wageni" au
"expatriate". Mfano tofauti ya masaa Africa na China ni kubwa. Kama
unamfanyakazi kutoka China na wewe uko Nairobi ina maana kuna vikao itabidi
vifanyike usiku. Swali ni je kila mtu yuko tayari kufanya vikao usiku pasipo
kulipwa "over-time"?
Lakini pamoja na faida na changamoto zilizopo jambo
linaloonekana hapa ni kwamba kila kitu kinawezekana. Na binafsi nimejifunza
kwamba hata unapopitia changamoto katika maisha yako binafsi usielemewe sana na
ile changamoto pasipokuona mafundisho mengine ya maisha unayoyapata kutokana na
changamoto ile.
Kwa mfano unaweza ukaachwa na mume wako au mke wako
na ukafikiri dunia ndiyo imekwisha. Kumbe kitu ambacho hukijui ni kwamba
pengine kwa yeye kukuacha amekusaidia kuokoa maisha yako. Vipi kama michepuko
yake ingekuja kukupa sumu na kukuua kabisa. Lakini kwa sababu umeweka sana
akili yajko katika kuachwa na mume wako au mke wako ndio maana unashindwa kuona
umeepuka nini au umepata nini cha ziada kutokana na changamoto yako.
Kwa mantiki hiyo hata katikati ya janga la
COVID-19, usilemewe sana kuangalia ni watu wangapi wako karantini. Angalia pia
dunia imejifunza nini? Mfano kwa sasa hata marais wa nchi zinazoitwa dunia ya
kwanza wanasema "jamani akili zetu zimechoka kufikiria tufanye nini dhidi
ya janga la COVID-19 tunaomba ninyi wananchi mumuombe Mungu atuepushe).
Hii haijawahi tokea. Binadamu huyu analiyejiona
anaweza kila kitu sababu ya teknolojia! leo anasema muombeni Mungu? Tena
kiongozi wa dunia inayojiita "dunia ya kwanza"? Wanamuomba Mungu
ambaye aliumba dunia na wala hakusema nyie ni dunia ya kwanza na wale ni dunia ya
tatu? Leo wanasema "kilichobakia ni kumuomba Mungu?" Jamani acheni
Mungu aitwe Mungu! Lazima ujiulize mara mbilimbili kuwa kuna jambo hapa dunia
imejifunza
Lakini zaidi ya hapo? dunia imekuwa kitu kimoja.
Katikati ya janga la COVID-19 hata mahasimu na maadui wameungana kupingana na
adui mmoja "the common enemy" kirusi kiitwacho CORONA. Hebu kumbuka
uhasama wa Marekani na China kuhusu "biashara". Uhasama wa Marekani
na Iran kuhusu "mambo yasiyojulikana". Nani leo anakumbuka mambo
yasiyojulikana? Hakuna ndugu yangu kila mtu anakumbuka Corona tu na kunawa
mikono!
Ndio maana leo hii hata wamarekani wanajitahidi
kujifunza kutoka China. Wanajiuliza hawa wachina wamefanya nini mpaka
maambukizo yameenda chini kiasi hiki? Hakuna anayechagua rafiki ni nani adui ni
nani? Kilichobakia ni kupambana na kirusi-Corona! Iwe ni Iran imeshusha
maambukizi? iwe ni Sudani? Iwe ni Israel? Iwe ni Afghanistan tutajifunza tu!
Na ajabu zaidi hata wale waliokuwa wakibeza kwamba
Afrika hamjielewi ndio maana magonjwa mengi yanawatafuna kuanzia Ebola, Utapia
Mlo mpaka HIV/AIDS leo wamejifunza kwamba sio suala la Afrika wala Ulaya wala
Amerika. Ni suala la uhai wa watu bila kujali utaifa, rangi, dini hata kabila.
Kama Mungu anavyotujali. Wakati wewe unaona yule ni...na yule ni...Mungu yeye
anaona hawa ni viumbe niliowaumba. Hili nalo dunia imejifunza bila kupenda. Ni
faida!
Kabla sijamaliza nikuchekeshe kitu. Lakini cheka
ukijifunza. Leo nikakutana na kaka yangu Daudi mmiliki wa Break-Point.
Alinikuta nimetoka kunawa mikono nikitokea jengo la IPS pale karibu na mnara wa
askari. Nikamwambia; "Ee Daudi dunia ingekuwa inanawa mikono namna hii
siku zote nani angekufa na kipindupindu? Akacheka sana! Lakini huo ndio
ukweli!Hata baada ya COVID-19 tuendelee kunawa mikono. Nani anayejua umeshika
nini ulipoenda maliwato!
Mengi yatazungumwa, mengi tutayaona, mengi
tutayasikia, lakini je wewe kama wewe umejifunza nini? umebadilika katika nini?
Je katika shida yako ya ndoa umejifunza nini kutokana na COVID-19? katika shida
yako ya ajira, umejifunza nini kutokana na COVID-19. Katika mahusiano yako na
Mungu umejifunza nini kutokana na COVID-19? Katika mtaa wako umejifunza nini
kutokana na COVID-19 na hata katika shida yako ya biashara umejifunza
nini kutokana na COVID-19?
Ndugu yangu, jambo la msingi katika maisha ni kujua
kwamba hata katika shida yako bado kuna mambo mengi sana ya kujifunza-Paul R.K
Mashauri
No comments:
Post a Comment